2017-06-15 15:04:00

Kanisa Katoliki Ugiriki laomba kusaidiwa kusaidia wahamiaji


Kuna hitaji la kupata msaada zaidi kutoka majimbo ya Ulaya kwenda kwa Kanisa Katoliki nchini Ugiriki katika harakati za kuwahudumia wahamiaji. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Ulaya kuwatambua waamini wa Ugiriki kuwa ni binadamu na sio takwimu. Askofu mkuu Sevastianos Rossolatos wa Jimbo kuu la Athens na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ugiriki, ametoa rai hiyo akiomba makanisa mengine Ulaya yalisaidie Kanisa nchini Ugiriki katika kuwahudumia wahamiaji.

Kanisa la Ugiriki linapitia kipindi kigumu kufuatia maamuzi mabovu kisiasa na myumbo wa uchumi nchini humo, changamoto zilizopelekea raia wengi wa nchi hiyo kujitoa uhai. Hali hii inatesa Kanisa la Ugiriki. Majimbo ya Ugiriki kwa kawaida yanajipatia kipato kutoka kwa wapangaji wa mali zisizohamishika zinazomilikiwa na majimbo hayo. Hata hivyo kwa hali iliyopo sasa, wapangaji wengi hawana tena uwezo wa kulipa kodi. Hivyo bajeti ya mwaka ya uendeshaji shughuli majimboni imeyumba.

Katika hali kama hiyo, wanajikuta kwa miaka mitatu sasa wanalazimika kuwakirimu na kuwahudumia pia wahamiaji, anasema Askofu mkuu Sevastianos Rossolatos. Kumekuwa na misaada kutoka shirika la Caritas la Barala la Maaskofu nchini Italia, na kwa watu wenye mapenzi mema. Hata hivyo kadiri ya takwimu, Kanisa nchini Ugiriki lina akiba ya kuweza kuhudumia wahamiaji kufikia mwezi Novemba 2017, baada ya hapo vichwa vinawauma maaskofu watakimbilia wapi.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.