Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Dumisheni uzalendo unaobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili

Watanzania jengeni uzalendo unaofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili, tayari kuzishuhudia ndani na nje ya Tanzania kama kielelezo cha imani tendaji! - REUTERS

15/06/2017 16:50

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo nchini Tanzania ni kipindimuafaka cha kumshukuru, kumtukuza na kumwomba Mwenyezi Mungu baraka na neema tele ili kweli Kanisa liendelee kujikita katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Katika kipindi cha miaka yote hii, Kanisa Katoliki nchini Tanzania limekuwa na kuongezeka maradufu, kwa kupata viongozi wazalendo pamoja na kuongezeka kwa Majimbo hadi kufikia 34 kwa wakati huu! Idadi ya waamini pia imeongezeka maradufu!

Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, licha ya kukua na kupanuka kwa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, lakini bado kuna changamoto kubwa katika kuanzisha na kuyategemeza Majimbo haya kwa: rasilimali fedha, watu na vitu; mambo yatakayosaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili! Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na familia ya Mungu nchini Tanzania, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linajitegemea katika maisha na utume wake!

Askofu mkuu Lebulu anasema, yote haya ni tisa, kumi na ambalo ni muhimu kuliko yote ni uzalendo wa Kikristo unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuvuka mipaka ya mahali anapotoka mtu, itikadi yake, hali yake ya kiuchumi na nafasi yake katika Jamii. Uzalendo wa Kikristo unabubujika kutoka katika imani kwa Kristo na Kanisa lake! Changamoto hii inapaswa kwanza kabisa kuvaliwa njuga na Maaskofu na wakleri waliopewa dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Tanzania. Waamini walei na watawa wanapaswa kujiuliza ikiwa kama wameiva katika uzalendo wa Kikristo kiasi kwamba, wanajisikia kuwa kweli ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa. Changamoto hii ipewe kipaumbele cha pekee, Kanisa la Tanzania linapojiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji ili kujenga na kuimarisha umoja, udugu na mapendo katika Kristo Yesu; ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ndani na nje ya Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

15/06/2017 16:50