Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Wimbi kubwa la watoto wahamiaji ni hatari sana kwa makuzi na usalama

Vita, ghasia, uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, umaskini, rushwa pamoja na athari kubwa za tabianchi jni kati ya mambo yanayochangia kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sanjari na watoto wasisindikizana na wazazi au walezi wao. - AFP

14/06/2017 08:10

Watoto wakimbizi na wahamiaji hasa wanaokuwa hawana watu wazima wanaosafiri nao, mara nyingi wanajikuta wakiishi kwenye hali duni sana na matumaini yao ya maisha ya baadaye yanafifia kwa kukosa huduma za elimu na afya. Hii ni sehemu ya Hotuba ya Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, Uswiss, akichangia hoja juu ya hali za watoto wakimbizi na wahamiaji pamoja na haki msingi za binadamu, kwenye kikao cha Baraza la haki msingi za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Watoto wakimbizi na wahamiaji ambao hawana watu wazima wa kuwaongoza katika mahangaiko yao, wamejikuta wakiwa wahanga wakuu wa biashara haramu ya binadamu, ngono holela na hatari zingine kama hizo zinazowapotezea kabisa mwelekeo wa maisha yenye utu. Kwa bahati mbaya sana kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko, watoto wakimbizi na wahamiaji wasio na walezi wakuwasindikiza kimaisha, hawana sauti na ni kama hawaonekani kwenye macho ya dunia, na watu wengi hawajali mahangaiko yao.

Hii ni kashfa kwa utu wa mwandamu na Jumuiya ya kimataifa inapaswa ifanye juhudi za kutosha ili kujibu mateso ya watoto hawa na kuwahakikishia haki zao msingi, kama ilivyo kwenye makubaliano ya haki za mtoto ya Umoja wa Mataifa. Katika kikao cha mwisho cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, Ujumbe wa Vatican walifanya kikao kidogo na Kamati Katoliki ya kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji, pamoja na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Kimataifa yaani Caritas Internationalis, ili kutafuta sababu zinazopelekea watoto wahamiaji kusafiri bila wazazi au walezi na nini kifanyike kukabiliana na changamoto hiyo.

Vatican inaendelea kutetea utu na haki msingi za kila binadamu bila kusita, na kusimamia sheria, kanuni na sera zenye mwelekeo wa kutetea hayo, na kwa namna ya pekee kabisa kwa watoto wahamiaji. Hivyo watoto hawa wapewe kipaumbele katika shughuli zote kitaifa na kimataifa ili kulinda utu na haki zao, anasema Askofu mkuu Ivan Jurkovic. Watoto wasichukuliwe kana kwamba ni bidhaa au wakosefu sababu tu ya hali yao ya uhamiaji au sababu wazazi na walezi wao ni wahamiaji. Ni binadamu wenye sura na mfano wa Mungu, wanastahili kupewa heshima na haki zao msingi. Kwa sababu hiyo ziepukwe tabia za kuwanyanyasa ikiwa ni pamoja na zile za kuwaweka chini ya ulinzi, kwani kitendo hicho hata kama ni cha muda mfupi, kina athari kubwa sana katika maisha yao ya baadae. 

Vita, ghasia, uvunjwaji wa haki za binadamu, rushwa, umaskini, na uharibifu wa mazingira ni kati ya sababu zinazopelekea watoto wahamiaji kusafiri bila wazazi au walezi wa kuwasindikiza. Mikakati yenye mwono wa mbali inahitajika ili kukabiliana na changamoto hii isiyovumilika hata kwa sekunde, ili kuwaokoa watoto wengi kutoka kwenye hatari mbaya za maisha wanazokumbana nazo, sababu wanalazimika kukimbia nchi zao na kuwa wakimbizi wakupoteza matumanai ya maisha yao ya baadae.

Watoto wanapaswa wahakikishiwe maendeleo endelevu ya maisha yao yanayoheshimu utu na haki zao. Vatican kwa kuzingatia hilo, inajikita kuwatazama kwa ukaribu watoto wote wanaoishi kwenye mazingira magumu katika nchi zao ili kuepuka wasiingiwe vishawishi vya kuanza kutangatanga kutafuta usalama, amani na fursa mahali pengine ambako hawana hata uhakika wa kupata wanachokitafuta. Askofu mkuu Ivan Jurkovic anasema, changamoto hii ya watoto wahamiaji wasio na wazazi au walezi wa kuwasindikiza, ni ishara ya ukosefu mkubwa wa usawa na kushindwa kwa mifumo. Hivyo ni lazima Jumuiya ya kimataifa kujichunguza upya ili kutafuta suluhu madhubuti za kuwahakikishia watoto hawa haki zao msingi na heshima kwa utu wao.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

14/06/2017 08:10