Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Katekesi siku ya Jumatano

Upendo wa Mungu hauna mipaka kwa waja wake!

Upendo ni chemchemi ya matumaini ya Kikristo kwani Mungu ni upendo!

14/06/2017 15:37

Mfano wa Baba mwenye huruma na Mwana mpotevu ni uhakika wa matumaini ya Kikristo, ndiyo tema iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 14 Juni 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mwana mpotevu baada ya kuchunguza dhamiri yake na kutambua kwamba, ametenda dhambi mbele ya Mungu, akajutia sana makosa yake na hatimaye, akaondoka kwenda kwa Baba yake ili kuomba msamaha wa dhambi zake. Lakini, Baba yake alipomwona kwa mbali akamwonea huruma, akakimbia kwenda kumlaki, akambusu, akamvika vazi jipya, viatu miguuni na pete kidoleni na nyumbani hapo pakawa hapatoshi, watu wakaanza kuselebuka kwenda mbele! Mwana mpotevu na yule kijana mkubwa aliyebaki nyumbani, wote wanapendwa na Baba yao na kwamba, wao ni chemchemi ya matumaini ya Kikristo!

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza katekesi yake, aliwatembelea na kuwasalimia wagonjwa na wazee waliokuwa wanafuatilia katekesi yake kutoka katika Ukumbi wa Paulo VI kutokana na jua kali wakati huu wa kiangazi hapa Roma. Baba Mtakatifu amewataka wagonjwa na wazee kufuatilia kwa makini Katekesi yake kwa njia Luninga, huku wakitambua kwamba, wote wameungana kwa pamoja. Huu ndio umoja wa Kanisa unaosimamiwa na Roho Mtakatifu. Wagonjwa na wazee, wamesali kwa pamoja ili kumwomba Roho Mtakatifu ili awaungaishe na kuwa wamoja. Baba Mtakatifu Francisko amewaweka wagonjwa na wazee wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Amewataka kuendelea kusali na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

14/06/2017 15:37