2017-06-14 16:23:00

Mjadala wa kimataifa kuhusu rushwa waanza Vatican


Kati ya vilema vya mfumo wa kidemokrasia, rushwa ya kisiasa imebobea kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba imekuwa ni saratani inayosaliti misimamo ya kimaadili na kanuni za haki jamii. Rushwa huujengea kashfa utendaji wa serikali kwa kusababisha mahusiano tenge kati ya viongozi wa serikali na wananchi wake. Rushwa inapelekea wananchi kutokuwa na imani na taasisi za serikali, kunawafanya wananchi kuchukia siasa na wawakilishaji wake.

Rushwa inaharibu mafungamano ya kijamii na husababisha huduma mbovu kwa wananchi. Matokeo yake ni kwamba, matakwa ya kisiasa yanapendelea maamuzi ya wale walio na uwezo pamoja na ushawishi wa kiuchumi na kwamba, maamuzi yao mara nyingi yanakuwa ni kikwazo katika kufikia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kwa kutambua athari za rushwa katika ustawi na maendeleo ya binadamu anasema Kardinali Peter Turkson, limeamua kuitisha mjadala wa kimataifa kuhusu rushwa. Huu ni mjadala utakaoendeshwa kwa kushirikia na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii.

Mjadala huu wa kimataifa, unazinduliwa, Alhamisi, tarehe 15 Juni 2017. Wajumbe wa mjadala wa saratani ya rushwa wanatoka katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu; mabalozi wanaowakilisha nchi na mashirika ya kimataifa mjini Vatican. Kardinali Turkson ameandika kitabu kuhusu “Rushwa” haya ni mahojiano maalum kati ya Kardinali Turkson na Bwana Vittorio V Alberti na Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuandika dibaji ya kitabu hiki, ambacho kinaanza kuwuzwa madukani, tarehe 15 Juni 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.