2017-06-14 13:43:00

Chansela Merkel, Bara la Afrika ni rasilimali na fursa kwa uwekezaji


Bara la Afrika ni rasilimali na fursa kubwa kwa Bara la Ulaya ambalo linakabiliwa na upungufu wa kizazi chenye nguvu kwa ajili ya kuendeleza jamii ya kesho Barani Ulaya. Kwa namna hiyo, kuna haja ya kulitazama Bara la Afrika kama fursa yenye rasilimali watu na vitu. Kwa mtazamo huu, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji inakuwa fursa ya kutengeneza wachapa kazi kwa ajili ya Bara la Ulaya, na kukuza mahusiano mazuri kati ya nchi za Ulaya na nchi wanakotoka wahamiaji hao, kwani Bara la Ulaya linahitaji nguvu kazi sio chini ya watu milioni 100 katika sekta mbali mbali. Haya ameyakiri Bi Angela Merkel, Chansela wa Ujerumani, alipokuwa na kikao na baadhi ya viongozi wa serikali kutoka Afrika, watakaoshiriki kwenye mkutano wa G20 mnamo tarehe 7 – 8 Julai, 2017.

Bara la Ulaya linatafuta namna ya kuziwezesha nchi za Afrika kusonga mbele, kukua, kujisimamia kisiasa, kiuchumi na kiusalama, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha vijana katika maendeleo ya kijamii nchini mwao. Kumbe katika hilo, Chansela Angela Merkel anaitazama changamoto ya wahamiaji kama fursa ya kutengeneza madaraja ya kukutana, kusaidiana na kushirikiana ili Mabara yote mawili, Afrika na Ulaya yaweze kupiga hatua kwa pamoja kwa mshikamano katika nyanja mbali mbali kimaisha.

Chansela Merkel anasema, serikali ya Ujerumani ipo tayari kuwekeza fedha zingine kiasi cha Euro milioni 300 kwenye nchi za kiafrika ambazo zitajitosa katika kuhangaikia haki msingi za binadamu ndani ya nchi zao. Bwana Paolo Gentiloni, Waziri mkuu wa Italia, kaweka wazi pia utayari wa serikali yake kuchangia katika maendeleo ya nchi za Afrika, hasa zile ambazo zinauhusiano wa muda mrefu na taifa la Italia. Hivi karibuni serikali ya Italia imeshiriki katika uanzishwaji wa taasisi mpya ya uchunguzi wa makosa dhidi ya kodi na fedha nchini Kenya. 

Viongozi wa nchi za Afrika walioko Berlin katika vikao hivyo wamepokea kwa furaha habari hizi za utayari wa Bara la Ulaya kuwa na ushirikiano na uwekezaji zaidi katika nchi za Afrika. Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali, ametahadharisha hatari ya jinsi Ugaidi unavyoshamili mahali palipo na umaskini na magumu mbali mbali ya kimaisha. Kwa hali hiyo anapendekeza Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia, kupambana zaidi kutokomeza ukosefu wa haki jamii katika nchi za Afrika. Kwa upande wake Rais Alassane Quattara wa Ivory Coast, amewashukuru viongozi wa serikali za nchi za Ulaya zilizo tayari kushirkiana na mpango wa Chansela Merkel kuhusu maendeleo endelevu ya Bara la Afrika.

Mpango wa Chansela Angela Merkel unalenga kukuza ushirikiano mkubwa wa kimaendeleo kati ya nchi za Mabara ya Ulaya na Afrika, pamoja na taasisi za fedha kidunia kufikia mwaka 2050, ambapo idadi ya wakazi Barani Afrika inatarajiwa kuwa imefikia bilioni 2.5. Katika kikao hicho cha kuboresha ushirikiano na mshikamano kati ya Mabara haya mawili, walikuwepo pia Bwana Jim Yong Kim, Rais wa Bank kuu ya dunia, na Bi Christine Lagarde, Mkurugenzi wa Shirika la fedha la kimataifa, ambaye anasema, kwa uzoefu wake, jamii yenye haki, amani, utawala wa sheria na inayopiga vita rushwa huvutia sana uwekezaji.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.