Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Ajira bado ni kizungumkuti duniani, waathirika zaidi ni vijana!

Ukosefu wa fursa za ajira unapelekea vijana wengi kuzikimbia nchi zao ili kutafuta fursa bora zaidi za maisha. - AP

14/06/2017 07:47

Kwa miaka kumi sasa soko la dunia limeonekana kushindwa kutengeneza fursa za ajira kwa nchi zilizoendelea na hata kwa maeneo ambapo kunakuibuka kwa masoko ya biashara mbali mbali. Hii inatokana na tatizo la kutokuwa na mfumo mzuri wa ajira na masoko, tatizo ambalo limekuwepo hata kabla ya myumbo wa uchumi. Kadiri hali ya ukosefu wa ajira inavyokua, kuna hatari ya watu kubanana kama ndizi mbovu sokoni, na kukata tamaa kwa kukosa ajira, hivyo kupelekea ongezeko la wakimbizi na wahamiaji.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, Uswiss, katika kikao cha kimataifa kuhusu hali ya ajira duniani, ameitahadharisha Jumuiya ya kimataifa kuhusu ukosefu wa usawa wa hali ya uchumi kwenye kila Bara, jambo linalopelekea hatari zaidi ya ukosefu wa ajira na kukua kwa makundi kwenye jamii kati ya wenye navyo na wale akina yakhe tia mchuzi pangu pakavu.

Dunia ina takribani watu milioni 200 leo wasio na ajira, kati yao vijana ndiyo wanaathirika zaidi. Wakati takwimu za mwaka 2015 zilionesha vijana waliokosa ajira na wanaoishi kwenye umaskini walikuwa asilimia 43%, takwimu za sasa zinaonesha kutangaza hali ya hatari zaidi kwani kuna vijana milioni 71 wasio na ajira, hali vijana milioni 156 ingawa wana ajira, bado wanaishi kwenye hali ya umaskini, kutokana na kipato cha chini cha ajira wanazozipata. Maendeleo ya sayansi na teknolojia, yanaelekea kuibua fursa mpya za ajira ambazo ni wazi zinahitaji zaidi ubunifu wa binadamu. Hata hivyo fursa hizi mpya zinaonekana kuja na hatari mbili ambazo zinapaswa kutathiminiwa kwa karibu sana, anasema Askofu mkuu Ivan Jurkovic.

Hatari ya kwanza ni kwamba teknolojia inaelekea kutumia Roboti zaidi katika shughuli mbali mbali ili kupunguza gharama na kujiongezea faida, jambo linalopelekea watu wengi kuachishwa kazi. Na wanaopoteza kazi sio tu walioichungulia shule kupitia madirishani, bali hata wale waliofanikiwa kujiendeleza kwenye fani za juu nao pia wamo mashakani. Hii itapelekea hatari ya kimazingira na kimaadili itakayotengenezwa na matumizi ya teknolojia mpya zinazobuniwa kwa sasa. Baba Mtakatifu Francisko anaonya kuwa, watu wasipoweka umakini wataishia kufanya kazi kwa kupingana, kila fani kutenda dhidi ya fani nyingine badala ya kushirikiana kidugu na kuboresha maisha ya Familia ya binadamu duniani kote.

Hatari ya pili ni ukweli kwamba, teknolojia mpya inahitaji weledi wa juu na umakini mkubwa, rasilimali ambazo asilimia kubwa ya watu katika jamii hawana. Suala hili litazidi kutengeneza pengo kubwa na ukosefu wa usawa kati ya watu. Hapo wa kuteseka zaidi ni wanyonge, na tatizo la kuyumba kwa viwanda litazidi kukua sababu ya uhitaji mkubwa wa weledi wa juu ambao wengi watashindwa kuufikia sababu ya gharama na uwezo. Hali hii itapelekea mvutano wa kimahusiano kati ya watu kwenye jamii. Elimu na mfumo wa malezi vitabidi viangaliwe upya ili kukabiliana na mabadiliko na changamoto kama hizi. Kanisa limekuwa likielekeza kila wakati kwamba elimu sio tu kwa ajili ya maendeleo ya mtu binafsi au kwa heshima ya utu wake, bali ni suala linalopaa juu zaidi ili kufikia kiwango cha kumwezesha mtu binafsi kushiriki kwenye jamii huru na kuwa chombo cha kukuza maelewano na urafiki kati ya watu wa mataifa, kabila na dini mbali mbali.

Suala la ajira na matokeo ya kazi kwa siku za usoni vitategemea sana juhudi na mwono wa pamoja. Kazi ni nyenzo ya maendeleo endelevu ya binadamu na hivyo kusaidia kufikia mahitaji matatu msingi ya binadamu: yaani, nia ya kukuza uwezo binafsi kiutendaji, nia ya kuhusiano na kushirikiana vema na wengine, na pia kujipatia kipato kwa ajili ya kujikimu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kazi inapaswa kutajirisha ukuaji wa mtu binafsi kiubunifu, mipango, vipaji, tunu na mahusiano ya watu. Kila shughuli za binadamu zinapaswa ziwe na mwelekeo wa mafao ya wengi, heshima kwa mali binafsi, mgawanyo wa rasilimali na majukumu, ushirikiano na mshikamano. Pale ambapo watu wanajali zaidi faida binafsi, ndipo ambapo kunakosekana heshima kwa viumbe, mazingira na utu wa mwanadamu. Askofu mkuu Ivan Jurkovic, ameialika Jumuiya ya kimataifa kuwa makini na ukuaji wa uchumi na teknolojia mpya duniani leo, kwani jamii itajikuta kwenye tatizo la ukosefu wa ajira kwa watu wengi na ukosefu mkubwa wa usawa kati ya watu. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kwamba katika maendeleo yote, utu na haki msingi za binadamu vinapewa kipaumbele ili kuunda jamii zenye usawa, amani na utulivu.

 

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

14/06/2017 07:47