2017-06-13 15:57:00

Waamini wanahamasishwa kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia!


Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 13 Juni, linaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Anthoni wa Padua, Padre na Mwalimu wa Kanisa: mhubiri mahiri wa Injili ya Kristo iliyomwilishwa katika huduma makini kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni changamoto kwa waamini kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa kwa kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiachilia na kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu na kamwe wasitafute njia za mkato katika maisha ya kiroho!

Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Frahncisko, wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 13 Juni 2017. Waamini wanaswa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, mambo msingi katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda makini kwa Kristo na Kanisa lake, kazi inayotekelezwa kwa ufanisi mkubwa na Roho Mtakatifu. Ushuhuda wa waamini unamtolea Mwenyezi Mungu sifa na utukufu, utimilifu wa changamoto za Kiinjili zilizotolewa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake hapa duniani.

Daima, Yesu alijitahidi kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni hapa duniani, akamtuma Roho wake Mtakatifu, ili aweze kuwapaka mafuta waja wake, tayari kwenda sehemu mbali mbali za dunia kutangaza na kushuhudia utukufu, ukuu na uweza Mungu katika maisha ya mwanadamu. Waamini wajitahidi kushuhudia mwanga uliomo ndani mwao, ili kumtukuza Baba yao wa mbinguni. Wawe ni chumvi inayokoleza utakatifu wa maisha, ili kufukuzilia mbali rushwa na ufisadi; mambo yanayowanyanyasa watu duniani. Waamini wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli kwa kusema “Ndiyo” na “Ndiyo” yao iwe imekamilika pasi na mawaa, kinyume cha hapo, kuna hila za Shetani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu ameliaminisha Kanisa lake kuwa ni chombo na shuhuda wa usalama na ukweli, kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; zawadi inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Ushuhuda usaidie kuyatakatifuza malimwengu, ili watu waweze kutembea katika mwanga wa maisha mapya. Waamini wasipokuwa makini, ushuhuda wao utakosa mvuto, dira na mwelekeo sahihi katika maisha na hizi ni dalili za kutokubali kumpokea Kristo Yesu na Roho wake Mtakatifu.

Waamini katika maisha yao, waendelea kujihoji ikiwa kama kweli wamekuwa ni mwanga wa Mataifa na chumvi ya ulimwengu kwa wale wanaowazunguka: Kumbe, huu ni wakati wa waamini kuwa ni mashuhuda wa mwanga wa Kristo Mfufuka. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, waamini waendelee kuwa ni mashuhuda wa utukufu na ukuu wa Mungu hapa duniani, ili watu wengine wanapoyaona matendo yao mema, waweze kumtukuza Baba yao wa mbinguni. Huu ndio ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema na baraka ya kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.