2017-06-13 07:23:00

Mateso na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Venezuela!


Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linasikitika sana kuona jinsi hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inavyoendelea kudidimia kila kukicha kiasi kwamba, sasa ghasia na vurugu; mauaji na nyanyaso mbali mbali zimekuwa ni chakula cha kila siku nchini humo. Kutokana na hali ya hewa kisiasa nchini Venezuela kuendelea kuwa tete, tarehe 8 Juni 2017, Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela lilikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekuwa karibu sana na wananchi wa Venezuela wanaoteseka kutokana na mipasuko ya kisiasa na kijamii nchini humo! Hotuba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela kwa Baba Mtakatifu Francisko ilitolewa na Askofu Diego Rafael Padron Sanchèz, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela.

Maaskofu wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo wa karibu, kwa huruma na upendo wake wa kibaba. Wanamshukuru kwa barua yake ya kidugu aliyowaandikia Maaskofu wote wa Venezuela kwa kuonesha masikitiko yake kuhusiana na kuporomoka kwa mustakabali wa demokrasia nchini Venezuela pamoja na mwendelezo wa machafuko ya kisiasa yanayosababisha mateso na mahangaiko kwa watu wasiokuwa na hatia. Machafuko haya kwa sasa yamefikia kipeo cha hali ya juu kiasi kwamba, serikali iliyoko madarakani imeamua kusimamia masilahi yake binafasi kwa kupambana na wale wote wanaotishia usalama na uwepo wake madarakani.

Serikali inatumia nguvu ya ziada kupambana na wananchi wa kawaida wanaodai uhuru, heshima na utu wao. Serikali imeamua kuitisha kura ya maoni mwishoni mwa Mwezi Julai bila ridhaa ya wananchi wenyewe na matokeo yake yanatarajiwa kuathiri mchakato mzima wa: uhuru na demokrasia nchini Venezuela. Venezuela itaanza kutawaliwa kwa mabavu; dhuluma na nyanyaso za kisiasa zitaongezeka na wapinzani watakiona kilicho mnyoa kanga manyoya! Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, katika utawala wa mabavu, rushwa na ufisadi vitaongezeka maradufu na matokeo yake ni kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema.

Ni hatari sana kwa uhuru wa kujieleza kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za nchi, hali ambayo pia itaathiri uhuru wa kidini. Ni kutokana na sababu hizi msingi, Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linapinga kwa nguvu zote, Bunge linalotarajiwa kufanya kikao chake mwishoni mwa Mwezi Julai, 2017. Majadiliano katika ukweli, uwazi, haki na amani yamechimbiwa chini na kufukiwa utadhani ni “makaburi”. Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linaishauri serikali kuanzisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi! 

Makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa kati ya Serikali na wapinzani mwezi Oktoba 2016 lakini yakashindwa kutekelezwa kwa sababu zisizofahamika yanaweza kuwa ni msingi wa majadiliano ili kurejesha tena ushiriki wa wananchi wengi wa Venezuela katika mustakabali na hatima ya maisha yao kwa sasa na kwa siku za usoni.  Katika hatua hii, Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linampongeza na kumshukuru Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa jitihada zake za kidiplomasia zilizopania kuhitimisha mpasuko wa kisiasa na kidemokrasia nchini Venezuela, kwa kuwaandikia barua wapinzani na serikali, hapo tarehe 1 Desemba 2016, lakini juhudi zote hizi zikagonga mwamba, Venezuela ikajikuta inatumbukia katika machafuko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Kama hali hii haitapewa ufumbuzi wa kudumu, kuna hatari kwa Venezuela kutumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe!

Wakati Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela likieleza mateso na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Venezuela, Baba Mtakatifu Francisko alikaa kimya, akawasikiliza kwa makini. Maaskofu wanakaza kusema, wananchi wengi kwa sasa wanakabiliwa na umaskini mkubwa wa hali na mali; wanateseka kwa baa la njaa na utapiamlo mkali kwa watoto; hawana tena huduma makini ya afya, kumbe, watu wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na magonjwa ambayo pengine yangeweza kutibika! Serikali inatumia nguvu kubwa kupambana na wananchi kiasi kwamba, kila siku kuna idadi kubwa ya watu wanaopoteza maisha na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela limemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kutokana na dhuluma, nyanyaso na hali tete nchini mwao, wakleri, watawa na waamini wamejikuta wakiwa wameunganika zaidi, kuliko wakati mwingine wowote wa historia yao, ili kutoa ushuhuda wenye mvuto kwa Kristo na Kanisa lake. Wao wanataka kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo, mshikamano katika kupambana na umaskini kwa wananchi wote wa Venezuela. Waamini wamekuwa mstari wa mbele katika maisha ya sala, ili kuomba huruma na upendo kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Venezuela.

Baraza la Maaskofu Katoliki limehitimisha ujumbe wake kwa Baba Mtakatifu Francisko, kwa kumtakia heri na baraka katika maandalizi na hatimaye, hija yake ya kitume nchini Colombia, mwezi Septemba, 2017. Kanisa linaendelea kufanya hija na waamini wote nchini Venezuela. Kwa mara nyingine tena, Maaskofu wanampongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa ajili ya kuwatetea wanyonge, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Ujumbe wake kwa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, maridhiano, utu, heshima na mafao ya wengi, umekuwa ukiwatia shime ya kusimama kidete kwa ajili ya kutetea utu na heshima ya binadamu pasi na ubaguzi!

Askofu Diego Rafael Padron Sanchèz, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema, hali tete ya Venezuela inaeleweka sana kwa Baba Mtakatifu Francisko. Ametumia fursa hii kuweza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Kanisa nchini Venezuela kwa ajili ya kurejesha tena misingi ya haki, amani, maridhiano na demokrasia ya kweli inayoheshimu utashi wa familia ya Mungu. Mpasuko wa kijamii, kisiasa na na kiuchumi usiwe ni sababu ya maafa makubwa kwa watu nchini Venezuela wanaohitaji msaada wa chakula, dawa, uhuru na demokrasia ya kweli.

Kwa upande wake, Kardinali Jorge Urosa Savino, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Caracas anasema, mkutano wao na Baba Mtakatifu Francisko umeimarisha umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa mahalia na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kujenga na kudumisha: imani, matumaini, mapendo na mshikamano wa dhati, ili kweli Venezuela iweze kupata ufumbuzi wa matatizo na changamoto ziliko mbele yake kwa wakati huu. Baba Mtakatifu bado anaendelea kukazia umuhimu wa majadiliano ya kisiasa katika ukweli na uwazi, kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu, ustawi na mafao ya wengi nchini Venezuela. Haya ni mambo msingi yanayoweza kutoa ufumbuzi wa kudumu nchini Venezuela.

Amani na utulivu nchini Venezuela inaweza kupatikana iwapo wananchi wataweza kupata chakula, huduma ya elimu na matibabu; uhuru wa kujieleza pamoja na uhuru wa kidini mambo msingi yanayodumisha utu na heshima ya binadamu. Vita ya wenyewe kwa wenyewe au mapinduzi ya serikali ni mambo ambayo hayana mashiko, kwani hakuna amani ya kweli inayoweza kupatikana kwa ncha ya upanga! Wananchi wanataka misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu iweze kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.