2017-06-12 15:55:00

Waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo vya faraja na huduma kwa jirani


Faraja ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huduma makini kwa jirani, changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na vyombo vya faraja ya Mungu kwa jirani zao. Ili kuwa kweli ni vyombo vya faraja na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kuna haja ya kuwa na moyo wazi, upole na unyenyekevu tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wahitaji badala ya kuwa na moyo mgumu wa jiwe unaooneshwa na watu wasiokuwa na haki!

Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote afarijiye watu katika dhiki, ili wao pia waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa faraja. Ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 12 Juni 2017. Faraja anasema Baba Mtakatifu ni mang’amuzi ya maisha ya kiroho! Hakuna mtu awaye yote anayeweza kujifaji mwenyewe, vinginevyo ni kujitafuta mwenyewe katika ubinafsi kwani faraja ni zawadi inayotolewa katika huduma kwa ajili ya ukuaji na ukomavu.

Katika Injili Kristo Yesu anaonesha watu waliomezwa kwa ubinafsi, kama: walimu wa sheria na wakuu wa makuhani! Tajiri aliyependa kujibovusha kwa kupenda tafrija na anasa, akawageuzia kisogo akina Lazaro Makini. Mafarisayo waliokuwa na sala ndefu na kudhani kwamba, kwa njia hii wanasikilizwa zaidi na Mwenyezi. Ni watu waliowakejeli wanyofu wa moyo, wakatafuta kujikweza! Baba Mtakatifu anakaza kusema, faraja ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kutumiwa kwa ajili ya huduma makini, kwani Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya faraja kwa waja wake; anayewahamasisha waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa faraja yake kwa watu wanaoteseka!

Faraja inafumbatwa katika maisha ya watu wanyenyekevu na wanyofu wa moyo, ili kufarijiwa na hatimaye, kutoa faraja kwa wengine. Kumbe, kimsingi: faraja ni zawadi kwa ajili ya huduma kwa watu wanaoteseka katika maisha! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake, anayewataka kuwa na nyoyo wazi zinazobubujika furaha katika umaskini wa roho, huzuni, upole; njaa na kiu ya haki; rehema na moyo safi; wapatanishi na wenye kuudhiwa kwa ajili ya upendo na haki. Kwa njia hii, waamini wanaweza kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya faraja ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasikika kusema, kwa watu ambao wana mioyo migumu iliyojifunga ndani mwao, wanadhani kwamba, wanajiweza kwa kujitegemea kwa kila jambo na kwamba, hawana sababu ya kuambata Heri za Mlimani; ni watu wakorofi na wanaochochea machafuko katika jamii; ni watu wasiokuwa na upendo wala huruma; ni wakatili wa kutupwa! Ni watu ambao kamwe, hawawezi kupokea wala kutoa msamaha, kwani wao wamegeuka kuwa ni vyombo vya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; tayari kushiriki katika nyanyaso na dhuluma kwa watu wengine. Hawa Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni watu wasiokuwa na furaha ya kweli, waliojificha na kujifunga katika ubinafsi wao, kiasi kwamba wanakosa zawadi ya faraja kwa jili ya huduma kwa jirani zao. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi, kufungua mioyo yao ili kupokea zawadi ya faraja, ili waweze kuitumia kwa ajili ya huduma makini kwa watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.