2017-06-12 16:09:00

Waamini: Onesheni upendo kwa Yesu na Ibada kwa Bikira Maria!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 10 Juni 2017 amewapigia simu washiriki wa maandamano ya Hija ya 39 ya Matembezi ya Miguu kutoka Macerata hadi Loreto, nchini Italia ili kuwatia shime katika hija yao! Hili ni tukio ambalo limefanyika mara tu baada ya kuwasili Mwenge wa Amani alioubariki mwenyewe, Jumatano tarehe 7 Juni 2017 wakati wa Katekesi yake kwa Siku ya Jumatano! Kardinali Kevin Joseph Farrel, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya washiriki wa matembezi haya ya kilometa 30, kama alama na ushuhuda wa Ibada kwa Bikira Maria.

Maandamano haya kwa mwaka 2017 yameongozwa na swali msingi kutoka kwa Yesu, Je, Simoni Petro, wanipenda? Baba Mtakatifu Francisko anawaambia waamini kumuuliza swali hilo Yesu, ikiwa kama anawapenda jinsi walivyo kwa kufikiri, kutenda na kutekeleza yale anayowaamuru kufanya? Anawataka waamini kujiabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwaombea na kuwafariji hasa wale wanaotoka katika maeneo ambayo yameathirika kutokana na tetemeko la ardhi lilitokea hivi karibuni nchini Italia.

Kardinali Kevin Joseph Farrel katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee waamini kutambua umuhimu wa hija ya maisha ya kiroho inayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; umoja na mshikamano kati ya waamini na Muumba wao; kwa kuwa ni vyombo vya huruma na upendo kwa jirani zao, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Licha ya udhaifu na dhambi za binadamu, lakini Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuwa mwaminifu kwa ahadi zake. Waamini wajitahidi kujenga na kudumisha urafiki na udugu pamoja na Kristo Yesu anayewakirimia dawa ya maisha ya kiroho, inayoganga na kuponya majeraha ya ndani! Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu daima anafanya hija na waja wake, kwa kuwaganga na kuwaponya madonda yao ndani, tayari kuwaumbia moyo mpya unaojenga umoja, upendo na mshikamano wa dhati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.