2017-06-12 15:29:00

Papa. Uchunguzi, Mazungumzano na Kujitosa kuwahudumia Wahamiaji


Serikali zina wajibu wa kutoa suluhu zanye kuzaa matunda katika kushughulikia changamoto ya wakimbizi na wahamiaji. Haiwezekani hata kidogo kuziba masikio kutokukisikia kilio cha watu wanaoishi katika mazingira yanayodharirisha utu wao. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Bi Blanca Alcalá, Spika wa Bunge la Bara la Amerika ya kusini na Carrebian, lililojumuika mjini Panama kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anaendelea kuitazama changamoto hii kama maisha halisi ya kila siku ya baadhi ya watu wanaoathiriwa na kinzani za kisiasa, kikabila, hali ya uchumi, mabadiliko ya tabia nchi, biashara haram ya binadamu na mambo mengine kama hayo. Mwaliko wa kutazama zaidi mapungufu na vidonda vya wale wanaoteseka kila siku kwa changamoto hiyo.

Ingawa ni muhimu kufahamu takwimu na ukweli wa changamoto ya wakimbizi na wahamiaji, isitazamwe kana kwamba ni suala la kufanyia utafiti, bali ni uhalisia wa maisha ya mateso makubwa kwa baadhi ya watu, ambapo kila mmoja ana historia yake, utamaduni, na matarajio, mambo ambayo yanapaswa kuthaminiwa na sio kuyatupilia mbali na kupoteza matumaini ya watu hawa, au kukanyaga heshima na utu wao. Takwimu na tafiti zinazofanyika, zisaidie kushiriki uhalisia wa maisha na hisia za watu hawa, ili kupata picha halisi itakayosukuma kila mmoja kutafuta suluhu ya kudumu kutokomeza changamoto hii.

Baba Mtakatifu Francisko anatumia maneno matatu yawe kama msukumo kwa viongozi wa serikali katika Bara la Amerika ya kusini na visiwa vya Carebian, kuhangaikia wakimbizi na wahamiaji ili kupata suluhu ya kudumu. Kwanza kabisa ni kuanza na tathmini ya uhalisia wa ukimbizi na uhamiaji kwa kufahamu vyanzo vyake. Uchunguzi huo usaidie kufikia hatua ya pili ambayo ni mazungumzano, ambapo kunakuwa na mahusiano mazuri kati ya watu, kuamsha mshikamano na wale wanaodhulumiwa haki zao msingi, na kukuza hali ya kuwajibika ili kuwarudishia hadhi yao. Kisha tatu, bidii ya kila mmoja na kwa pamoja kushirikiana ili kutengeneza mipango mikakati yenye usawa katika kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Upatikanaji wa muafaka katika makubaliano ni sanaa ya msingi inayohitaji umakini mkubwa.

Lazima kuhakikisha viongozi wa serikali mahalia na Jumuiya ya kimataifa, wanapata nyenzo msingi katika kuboresha makubaliano kwa ajili ya mafao ya wengi, na hasa wale walio katika hali za unyonge zaidi. Ili kutokomeza janga la biashara haram ya binadamu na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji, ni muhimu kutokuwachukulia kama bidhaa bali binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Shughuli hii ni nzito inayohitaji wanaume na wanawake wanaojitosa kimasomaso kuhakikisha suluhu ya kudumu inapatikana, anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.