2017-06-12 11:00:00

Papa Francisko asema: Upendo ni muhtasari wa Fumbo la Utatu Mtakatifu


Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote! Hii ni baraka na mang’amuzi ya Mtakatifu Paulo yanayowasaidia waamini kuweza kulitafakari kwa kina Fumbo la Utatu Mtakatifu linalofumbatwa katika upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Yesu Kristo Mfufuka, ulioleta mageuzi makubwa katika maisha ya Mtakatifu Paulo, kiasi hata cha kumsukuma kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema miongoni mwa watu wa Mataifa.

Uzoevu na mang’amuzi haya yanamwezesha Mtakatifu Paulo kuwahamasisha Wakristo kuwa na furaha, huku wakiendelea kukamilishana pamoja na kuishi kwa amani na maridhiano. Jumuiya ya Kikristo hata katika udhaifu wake wa kibinadamu inaweza kuwa ni kioo cha umoja unaofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kujikita katika wema na uzuri, mambo msingi yanayojikita katika huruma ya Mungu na msamaha wake kwa binadamu! Hii ni sehemu ya tafakari ya kina iliuyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 11 Juni 2017, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Katika hija ya maisha ya Waisraeli kutoka utumwani Misri, walielemewa na udhaifu wao wa kibinadamu kiasi hata cha kuvunja Amri na Maagano na Mwenyezi Mungu, lakini bado akaendelea kujifunua kuwa ni Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo, si mwepesi wa hasira na kwamba, ni mwaminifu kwa ahadi zake. Jina la Mwenyezi Mungu linaonesha uwepo wake wa karibu kati pamoja na watu wake na wala si Mungu anayejificha ndani mwake, bali ni maisha; na kwamba, anataka kuwasiliana na waja wake katika uwazi; ni Upendo unaomwokoa mwanadamu kutoka katika hali yake ya kukosa uaminifu.

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, mapendo na msamaha unaowawezesha binadamu kupata msamaha wa dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu, ili hatimaye, kuwaongoza na kuwaelekeza katika njia ya amani na ukweli. Ufunuo huu wa Mwenyezi Mungu unapata utimilifu wake kwenye Agano Jipya kwa njia ya mafundisho ya Yesu na utume wake wa ukombozi kwa mwanadamu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake amewafunulia wanadamu Uso wa Mungu Mmoja katika Nafsi Tatu, zinazofumbatwa katika upendo unaowaunganisha wote katika: kazi ya uumbaji, ukombozi na kutakatifuza yaani: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kuhusu mhusika mkuu katika Injili ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, inayomwonesha Nikodemo, mtu ambaye alikuwa na nafasi ya juu sana katika Jumuiya ya waamini, lakini bado aliendelea kujitaabisha kumtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha yake, kiasi cha kukutana na Yesu katika uficho na anatambua kwamba, hata kabla ya kuanza kumtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha yake, tayari Mungu alikuwa anamtafuta kwanza, kwani anawapenda na kuwajali waja wake. Ndiyo maana Injili inasema kwa uhakika kwamba, Mwenyezi Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanaye wa pekee, ili kila anayemwamini asipotee bali aweze kupata maisha ya uzima wa milele, ambayo kimsingi ni upendo usiokuwa na mipaka kutoka kwa Mwenyezi Mungu uliofunuliwa na Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba, kwa kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, upendo huu ni kazi ya Roho Mtakatifu anayeuangazia ulimwengu kwa mwanga wake na kila moyo wa mwanadamu unaoweza kuupokea mwanga huu unapata nguvu ya kufukuzia mbali giza na ugumu wa moyo unaokwamisha mchakato wa kuzaa matunda bora yanayosimikwa katika Injili ya upendo na huruma! Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni, anamwomba, Bikira Maria aweze kuwasaidia waamini kuzama zaidi katika umoja wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kuishi na kushuhudia upendo unaotoa maana ya maisha yao hapa duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.