2017-06-12 15:06:00

Msaada wa haraka wahitajika kufuatia baa la njaa Sudan kusini


Baraza la Maaskofu nchini Sudan limetoa rai kushughulikia kwa dharura hali ya mahitaji msingi ya binadamu kwa raia zaidi ya Milioni 4.9 kati ya wakazi Milioni 11 nchini Sudan ya kusini. Tarehe 20 Febbruari 2017, serikali ya Sudani ya kusini ilitangaza hatari ya baa la njaa kwenye maeneo mbali mbali, ambapo kuna zaidi ya watoto milioni moja chini ya miaka mitano, wanaoathirika kwa utapia mlo mkali.

Katika ujumbe wao wa kichungaji, Maaskofu wa Sudan wanaialika Jumuiya ya kimataifa, kuingilia kati kwa haraka iwezekanavyo kutatua changamoto ya baa la njaa, vingninevyo hali inaelekea kuwa mbaya zaidi. Inapozingatiwa nchi hiyo imo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013, hali halisi za maisha ya raia zinaonekana kudhoofika na kuwa hatarini siku hadi siku. Ghasia za kisiasa nchini Sudan ya kusini, zimepelekea takribani watu milioni 3 kuikimbia nchi yao na kutafuta hifadhi kwa nchi majirani.

Ghasia hizo za kisiasa zinaligusa pia Kanisa nchini humo, kwa namna ya pekee makasisi na watawa wa kike na wa kiume. Maaskofu katika ujumbe wao kwa waamini nchini mwao, wameeleza kwa masikitiko pia kwamba kuna baadhi ya makanisa yamechomwa moto. Maaskofu wamesisitiza kwamba katika ghasia za kisiasa nchini mwao hawafungamani na upande wowote kati ya wanaokinzana. Kanisa linatetea haki, amani, huruma, upatanisho, mazungumzano, taifa la utaratibu wa sheria na utawala bora. Kwa sababu hiyo, Kanisa litaendelea kupiga vita ghasia, ubaguzi, rushwa na ukandamizaji. Maaskofu wanapenda pande zote zinazokinzana zitambue kwamba Kanisa litabaki na msimamo huo na kusonga mbele bila kigugumizi hata kama wanajaribu kulifanya litembee kwa kuchechemea kutokana na kuathirika na ghasia hizo.

Maaskofu nchini Sudan katika ujumbe wao wamekumbusha maneno ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoyazungumza hivi karibuni wakati wa Katekesi yake: habari kutoka Sudani ya kusini zinaleta maumivu makali ambapo pamoja na vita ya wenyewe kwa wenyewe kama ndugu, sasa kunaongezeka baa la njaa ambalo linapelekea vifo vya mamilioni ya watu, kati yao watoto ni wengi sana. Baba Mtakatifu Francisko, amewaalika wote wenye mapenzi mema, kutoishia kuzungumza tu, bali kupiga hatua zaidi kuhakikisha mahitaji msingi na hasa lishe yanawafikia wakazi wa nchi hiyo.

Sudani ya kusini limekuwa taifa linalojitegemea tangu 2011. Mwaka 2013 likajikuta likitumbukia kwenye vita ya wenyewe kwa kwenyewe. Vita ambayo imepelekea vifo vya mamilioni ya watu, ingawa zimekuwepo juhudi za misaada mbali mbali kuwahangaikia wananchi wa taifa hilo. Baba Mtakatifu Francisko, anatoa mwaliko kuwaombea raia wa taifa hilo, pamoja na wote wanaohangaika usiku na mchana ili kutatua changamoto zao na kuboresha maisha yao, Bwana awatie nguvu na kuwaongoza kuelekea mafanikio ya matamanio mema, kwa ajili ya Sudani ya kusini yenye amani, heshima na utulivu.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.