2017-06-10 07:00:00

Usiridhike, jitose zaidi kuhangaikia Wakimbizi na Wahamiaji


Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ni fursa ya kujenga madaraja ya kukutana kati ya watu, kuishi mshikamano, kufufua utamaduni wa kuaminiana na kutiana moyo katika utendaji wa pamoja. Jamii ya leo inahitaji wanaume na wanawake watetea amani, wenye mwono na uhamasishaji wa pamoja. Patriak Bartolomeo I wa Kanisa la Constantinopoli katoa rai hiyo kwenye kikao cha maridhiano cha Umoja wa Ulaya, akizialika taasisi barani Ulaya zijitose zaidi katika kuhudumia wakimbizi na wahamiaji.

Barani Ulaya kwa ushirikiano wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, kumekuwa na jitihada za kampeni zijulikanazo kama “Pamoja na Wakimbizi”, With Refugees, zenye lengo la kuhamasisha wahamiaji kujisikia sehemu ya jamii walimojikuta kwa sasa. Kumekuwa na mashindano ya kimichezo, tamasha za muziki, vyakula vya pamoja na maonesho mbali mbali yanayowahusisha wakimbizi kama sehemu ya jamii walizomo. Hata hivyo Patriak Bartolomeo anasisitiza kwamba kuna haja ya kufanya zaidi.

Kikao cha maridhiano cha Umoja wa Ulaya kimefanyika hivi karibuni huko Athene, nchini Ugiriki kikiongozwa na kauli mbiu “Uhamiaji changamoto kwa utambulisho wa Bara la Ulaya”. Patriak Bartolmeo I anasisitiza kila serikali, taasisi, dini, na mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya kazi kwa pamoja kila mmoja akizingatia wajibu wake ili kuwalinda na kuwahangaikia walio wanyonge katika kuleta tena tumaini la kuboresha hali za watu katika jamii.

Changamoto ya wahamiaji sio ya Bara la Ulaya peke yake bali ni changamoto ya dunia nzima, kwani ni changamoto inayogusa miili na mioyo ya wanadamu, uhuru, utu na utakatifu wao. Kwa sababu hiyo vita dhidi ya unyanyasaji, ukandamizaji, ubaguzi, na unyonyaji inapaswa kuwa ni vita inayogusa kila jamii duniani na kila mwanadamu, anasema Patriak Bartolomeo. Hivyo ni muhimu kubadilisha tishio la uhamiaji kuwa nafasi ya kujenga utamaduni wa mshikamano na ushirikishanaji. Serikali zinapaswa zitazame taasisi za dini kama wadau wa kushirikiana nao bega kwa bega kwani ni taasisi zenye nafasi ya msingi katika maisha ya watu binafsi na zinawakilisha nafasi kubwa ya tumaini la jamii.

Kwa mantiki hiyo, ni muhimu kutengeneza fursa za mazungumzano kati ya watu wa dini mbali mbali, na kati ya taasisi za dini na serikali ili kuwepo na hali nzuri ya kuishi kwa pamoja kwa amani na kuheshimiana, kushikamana, kuaminiana kwa namna ambayo kwa pamoja wataweza kukabiliana na changamoto ya wakimbizi na kuifanya kuwa ni fursa ya kuheshimu utu wa mwanadamu katika uhuru na haki.

Changamoto ya wahamiaji inagusa kwa namna ya pekee utambulisho wa Bara la Ulaya. Bara linalojipambanua kwa utamaduni wa kikristo, kwa kutetea haki za binadamu, lakini cha kushangaza hao hao wanaonekana kutumia lugha kali dhidi ya wakimbizi na wahamiaji, na zaidi sana wanataka kufunga mipaka, kujenga kuta za kuzuia wakimbizi kupata hifadhi katika jamii zao. Jambo hili haliwezi kukubalika hata kidogo, ni kupoteza utambulisho wa Bara la Ulaya, anasisitiza Patriak Bartolomeo.

Hivyo hivyo haiwezekani kuifikiria jamii ya Ulaya kiteknolojia, kiuchumi, kidemokrasia na kiusalama peke yake bila kutumia nyenzo za msingi kama heshima, haki na ukarimu. Mtume Paulo anafundisha: Hata kama nikinena lugha za watu na hata za malaika, lakini kama sina upendo mimi nimekuwa kama sauti ya debe tupu au kengele. Tena, naweza kuwa na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, nikafahamu siri zote na kujua kila kitu; naweza kuwa na imani yote hata nikaweza kuhamisha milima, lakini kama sina upendo mimi si kitu” (IWakoritho 13: 1 -2). Hivyo huwezi kutenganisha uhangaikiaji wa amani na usalama bila kujali utu na haki za binadamu kwa upendo. Kila mwanadamu atambuliwe kuwa ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na maendeleo endelevu ya binadamu huyo yanapaswa yazingatie pia utunzaji bora wa mazingira.

Ukarimu kwa wahamiaji ni kiini cha utume wa Kanisa katika jamii ya leo. Akitoa mfano wa msamaria mwema, Patriak Bartolomeo anaalika kila mmoja awe jirani mwema, msamaria mwema kwa wahamiaji wanaolazimika kwenda mbali na kutengana na watu wao wa karibu, kutengana na utamaduni wao, siasa zao, na taifa lao. Haiwezekani kuziba masikio kutokukisikia kilio cha wakimbizi na wahamiaji. Tarehe 20 Juni, dunia nzima itaadhimisha siku ya wakimbizi na wahamiaji ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wajibu wa kila mmoja katika kuwajali na kuwahangaikia wale wote wanaotafuta hifadhi katika jamii ngeni wakikimbia vita, unyanyasaji, na hali ngumu ya maisha sehemu zao asilia.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.