2017-06-10 14:28:00

Sinodi Buenos Aires, Kanisa linalotoka kukutana na watu


Msukumo wa uinjilishaji mpya, majadiliano ya kujenga, utajiri unaofumbatwa katika umoja na utofauti, kupendelea maskini, sala, usikilizaji, unyenyekevu, uwazi katika kuchagua njia ya uinjilishaji, roho ya umoja kama kanuni ya uelimishaji na namna ya utendaji kutoka moyoni, ni baadhi ya maneno-funguo yanayotumiwa na Kardinali Mario Aurelio Poli, Askofu mkuu wa Buenos Aires, katika Barua yake ya kichungaji wakati wa shamrashamra za Pentekoste, kama mwongozo wa Sinodi ya kijimbo itakayofanyika kati ya mwaka 2017 na 2019. Hitimisho la Sinodi hiyo kijimbo litaenda sambamba na sherehe za miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Buenos Aires (1620 – 2020).

Kardinali Poli anakumbusha umuhimu wa Roho Mtakatifu katika shughuli zote za sinodi, kwani ndiye mtendaji mkuu na rafiki mwaminifu ambaye wabatizwa wote wanamhitaji katika hija yao ya maisha. Sinodi maana yake ni kutembea pamoja, njia ya Kristo inayowapeleka waamini kwa Mungu Baba. Sinodi jimboni Buenos Aires itafanyika kwa kuzingatia pia utume wa Baba Mtakatifu Francisko, ambapo mwanga wake unapatikana katika Barua ya Kitume, Evangelii gaudium, Furaha ya Injili. Sinodi itakayokuwa na mwelekeo wa umisionari wenye lengo la kubadili kila kitu, kiasi cha kufanya tamaduni, mitindo ya maisha, ratiba, lugha na kila mfumo wa Kanisa kuwa mkondo stahiki kwa ajili ya kuinjilisha, na sio tu kujilinda kiimani.

Wakiongozwa na msukumo huo, Kardinali Poli anawaalika mapadri, mashemasi, wenye maisha ya wakfu, na kila mdau wa uinjilishaji awe tayari kusikiliza na kushiriki kikamilifu katika kutafuta changamoto na mahitaji msingi ndani ya Jumuiya ya wakristo Jimboni Buenos Aires. Hali ya Jimbo kuu la Buenos Aires kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii hasa vijana na watoto. Kutokana na ukosefu wa usawa katika sekta nyingi kunapelekea ghasia kubwa katika jamii hiyo, wakati mwingine zikisababishwa na ukosekanaji wa mahitaji msingi kabisa ya binadamu kwa ajili ya kuishi.

Katika hali kama hii, imani ya kikristo ni ya msingi sana katika kujenga vifungo vya kifamilia na udugu kati ya watu, tunu ambazo zimerithishwa katika jamii ya Argentina kwa vizazi vingi sasa. Ni mwaliko wa kutembea na nguvu ya Injili ili kujenga mshikamano unaoshinda kila aina ya nadharia. “Tunahitaji Kanisa maskini kwa ajili ya maskini”, amesisitiza Kardinali Poli katika barua yake ya kichungaji.

Maskini wanayo mengi ya kuifundisha jamii ya leo hasa waamini, kwani mbali ya kuishi katika maumivu, wanamfahamu pia Kristo msulubiwa. Hivyo ni muhimu kila mwamini na wanadamu wote waruhusu kujifunza na kuinjilishwa kutokana na mahitaji na maisha ya maskini. Kardinali Poli anahamasisha utamaduni wa kusikiliza katika Kanisa lenye utii wa imani, linalotafsiri Neno la Mungu katika matendo. Utamaduni wa kusikiliza unajengwa kwa kuwasogelea wengine, katika maisha yao ya kila siku bila maamuzi mbele, na kwa lugha yenye heshima. Sinodi ya Jimbo kuu la Buenos Aires ina mwelekeo wa kumpeleka Kristo kati ya wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi cha kujitambua kuwa ni Kanisa linalotoka ili kukutana na watu.

Sinodi ya Jimbo kuu la Buenos Aires inatarajiwa kuhitimishwa mwaka 2019 wakati wa kipindi cha majilio, sambamba na ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 400 tangu kuanzishwa Jimbo hilo. Sinodi itagawanyika katika hatua tatu: mosi itakuwa kusikiliza Roho Mtakatifu kupitia waamini ili kufahamu mahitaji ya kijimbo kwa karne hii, pili itakuwa kuutambua uso wa Kristo kwa jirani kwa kuchanganua vipaumbele, na tatu itakuwa kutambua mapenzi ya Mungu katika shughuli za uinjilishaji jimboni humo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.