2017-06-10 17:07:00

Sherehe ya Utatu Mtakatifu: Umoja, upendo na mshikamano wa dhati!


Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na pendo la Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote! Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican ukweli uliofunuliwa wa Utatu Mtakatifu umekuwa ni chemchemi ya imani hai ya Kanisa, hasa kwa njia ya Ubatizo; mahubiri, katekesi na katika Sala ya Kanisa. Kanisa linaungama Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja. Huu ni Utatu wa uwamo wa pamoja, yaani: Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kila mmoja wa Nafsi hizi Tatu ni ukweli huu yaani: uwamo na uwapo. Nafsi za Mungu zinatofauti ya kweli kati yao. Zina uhusiano wa moja kwa moja. Kumbe, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya: Umoja, Upendo na mshikamano wa dhati!

Kanisa linaadhimisha Fumbo la Utukufu na Ukuu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu wa milele katika kuungama imani ya kweli, na kuabudu Umoja wa Mungu katika enzi ya fahari yake. Kwa neema ya Ubatizo katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, waamini wanashiriki uzima wa Utatu Mtakatifu hapa duniani katika giza la imani na baada ya kifo katika mwanga wa milele. Imani ya Kanisa Katoliki ndiyo hii kwa ufupi: Kanisa linafundisha. ina amini na kumwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kuchanganya Nafsi, wala kutenganisha uwamo: katika Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Huu ni Umungu mmoja, utukufu ulio sawa, ukuu wa pamoja wa milele!

Katika tafakari hii, Padre Stefano Kaombe, kutoka Parokia ya Chang’ombe, Jimbo kuu la Dar es Salaam anatafakari kwa kina na mapana kuhusu Amri ya kwanza ya Mungu, inayowataka waamini kumwabudu Mungu peke yake! Lakini leo hii kuna miungu: fedha, mali, madaraka na uwezo wa kiuchumi. Lakini, waamini wanakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayestahili kusifiwa, kuabudiwa na kutukuzwa milele.

Padre Kaombe anagusia neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, upendo wa Mungu na ushirika wa Roho Mtakatifu, inayopaswa kukaa ndani ya waamini ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao kwa njia ya matendo ya huruma, kama Kanisa lilivyokazia wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni chemchemi ya upendo, umoja na mshikamano dhidi ya ubinafsi, tamaa, uchoyo na hali ya watu kujitafuta wenyewe! Upendo unafumbatwa katika sadaka na majitoleo kwa wengine ni sawa na mshumaa unaoteketea ili kutoa mwanga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.