Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Semina kuhusu: wahamiaji, wakimbizi na waathirika wa utumwa mamboleo

Kanisa linaendelea kupembua kuhusu matatizo, changamoto na fursa za wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani kwa wakati huu ili kumwezesha Baba Mtakatifu kutoka mwelekeo wa shughuli za kichungaji. - AFP

10/06/2017 16:19

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, kuanzia tarehe 12-13 Juni 2017 linaendesha semina ya kimataifa kuhusu wahamiaji, wakimbizi na waathirika wa biashara haramu ya binadamu. Zaidi ya wajumbe 40 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanashiriki, hawa ni Maaskofu na Makatibu watendaji wa Idara za wakimbizi na wahamiaji kutoka katika Mabara ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia pamoja wadau ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za waathirika wa biashara haramu ya binadamu!

Semina hii ni sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya kitengo cha wahamiaji na wakimbizi kutoka Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kuhusu madhara ya uhamiaji yatakayoidhinishwa katika kipindi cha mwaka 2018. Lengo la semina hii ni kutakaka kushirikishana matatizo, changamoto na fursa zinazojitokeza kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, kuna idadi kubwa ya watu wanaoomba hifadhi ya kisiasa; kuna waathirika wa biashara haramu ya binadamu pamoja na watu wasiokuwa na makazi ya kudumu hata katika nchi zao wenyewe! Changamoto hizi zinaaangaliwa kwa kina na mapana, ili hatimaye, kumshirikisha Baba Mtakatifu Francisko aweze kuzitolea mwelekeo wa kichungaji kwa ajili ya Kanisa zima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

10/06/2017 16:19