2017-06-10 14:13:00

CUAMM nchini Angola, huduma ya afya kwa wahitaji zaidi


Mnamo tarehe 13 Juni 1997 juhudi za dharura hasa kwa upande wa afya zilifanyika na madaktari kwa ajili ya Afrika, CUAMM, kusaidia umati wa watu walioathirika na vita ya wenyewe kwa wenyewe maeneo ya Uige, nchini Angola. Leo hii maeneo ya Chiulo kusini mwa nchi hiyo, kipaumbele kimeelekezwa zaidi kwa afya za akina mama na watoto. Padre Dante Carraro, mkurugenzi wa madaktari kwa ajili ya Afrika, CUAMM, anasema, wakati wanaenda kuhudumia waathirika wa vita mnamo mwaka 1997, vita hiyo ya wenyewe kwa wenyewe ilikuwa imedumu zaidi ya miaka 20 nchini Angola, na kupelekea mfumo wa afya kupasuka vibaya kiasi cha kuharibu hata mahusiano ya kijamii kati yao.

Mwaka 2002 amani iliporejea Angola, madaktari kwa ajili ya Afrika walianza mipango ya muda mrefu zaidi kwenye huduma za afya. Kumekuwa na mafanikio mengi lakini pia changamoto. Kati ya kumbukumbu za huzuni ni pamoja na kifo cha Nesi Marisa Ferrari aliyefariki kwenye ajali ya barabarani huko Chiulo mwaka 2004, kisha janga la ugonjwa wa Marburg ambalo liliondoka na Daktari wa watoto, Bi Maria Bonino, aliyewahangaikia watoto wa Uige hadi ilipomtoka pumzi ya mwisho.

Kwa sasa madaktari kwa ajili ya Afrika, CUAMM, wanatoa huduma kwa namna mbili nchini Angola. Kwanza wanashirikiana na wizara ya Afya katika kuendeleza juhudi za kutibu kisukari kwa wagonjwa ambao wameathirika na Kifuakikuu tangu 2014, na pili ni ushirikiano na Hospitali ya Chiulo tangu 2012, kwa lengo la kuhudumia zaidi akina mama na watoto ili kuhakikisha akina mama wanajifungua salama, wanakuwa na lishe bora wao na watoto wao, kwa muda wote tangu wakati wa ujauzito mpaka miaka miwili baada ya kujifungua.

Padre Dante Carraro anaendelea kusema kwamba, huduma na mafanikio yanayopatikana katika Hospitali ya Chiulo ni ushindi mkubwa na nyota ya kuangaza kama mfano katika kuhudumia wahitaji zaidi. Izingatiwe kwamba Hospitali hiyo ipo kwenye eneo ambalo ni nusu jangwa, ambapo akina mama wajawazito wanalazimika kutembea kilomita za kutosha chini ya jua kali kabla ya kufika Hospitalini hapo kujifungua. Takwimu za 2016 zinaonesha akina mama 1,700 walijifungua salama Hospitalini hapo, ambapo kuna vitanda 30 tu vya kujifungulia. Amani nchini humo iliyopatikana mwaka 2002 imekuwa ni neema iliyopelekea hata kufumuka na kukua kwa uchumi wa nchi ya Angola kufuatia biashara ya mafuta ya Petroli.   

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.