2017-06-09 15:25:00

Wanawake wanayo dhamana ya kuelimisha udugu duniani!


Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika mkutano wa Baraza uliofunguliwa tarehe 7 Juni 2017 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wanawake wanaelimisha udugu” anasema, wanawake wanapaswa kujengewa uwezo wa majadiliano yanayojikita katika uhalisia wa maisha ya watu kwa kuanzia katika familia. Hii ndiyo changamoto kubwa inayoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambamo kuna mwingiliano mkubwa wa tamaduni mbali mbali. Katika mazingira kama haya kuna haja ya kutambua na kuthamini mchango wa wanawake katika mchakato mzima wa majadiliano ya kidini! Kimsingi wanawake wamekirimiwa zawadi ya kufundisha, kuelimisha na kuwafunda watu!

Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mchango wa wanawake duniani, tangu pale haki zao msingi zilipoanza kutambuliwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa na jamii wanamoishi. Kardinali Tauran anasikitika kusema, katika jamii ambamo mfumo dume bado unatawala, mchango, dhamana na ushiriki wa wanawake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni kidogo sana na matokeo yake ni “vipigo vya majumbani”, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; ukeketaji; ukosefu wa usawa katika fursa za ajira na malipo; uwakilishi mdogo katika kupanga na kutekeleza majukumu mbali mbali ya kijamii! Kutambua na kuthamini utu na heshima ya wanawake, kuna maanisha kwamba, wanawake wanao mchango mkubwa katika mchakato mzima wa maisha ya hadhara!

Mkutano wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kwa Mwaka 2017 umetoa kipaumbele cha kwanza kwa wanawake kutoka katika medani mbali mbali za maisha ili kuchambua dhamana na nafasi ya wanawake katika kuelimisha udugu. Kwa upande wake, Clare Amos kutoka Baraza la Makanisa Ulimwenguni amekita tafakari yake kwa Kristo Yesu kuwa ni upatanisho kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu. Upatanisho ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Kuna haja ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli waamini wa dini mbali mbali waweze kuheshimiana na kuthaminiana kwa kukuza na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa kweli.

Mchakato huu pia hauna budi kuwagusa wanawake na wanaume ili waweze kujipatanisha, tayari kushirikiana katika kukuza na kudumisha upatanisho wa wote. Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upatanisho, haki na amani duniani, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Stefano, Shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya imani kwa Kristo na Kanisa lake! Yesu katika maisha na utume wake, alikuwa ni chachu ya majadiliano yaliyowagusa wale ambao kutokana na sababu mbali mbali walikuwa wametengwa na jamii kama ilivyotokea kwa yule Mwanamke Msamaria pale kisimani. Kumbe, wanawake washirikishwe kikamilifu katika mchakato mzima wa majadiliano ya kidini katika ngazi mbali mbali duniani!

Kwa upande wake Nuria Calduch-Benages, mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mataktifu kutoka Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregoriani amefafanua kuhusu uzoefu wa wanawake katika makuzi na uelimishaji wa udugu ndani ya jamii mintarafu Maandiko Matakatifu. Ameonesha mchango wa wanawake katika masuala ya kijamii, kisiasa na kisheria. Amekazia kwamba, hekima inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu ni chemchemi na chachu ya majadiliano ya kidini na kiekumene; chachu inayopaswa kusaidia mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Kitabu cha Hekima ya Sulemani, Zaburi na Mithali vinamwonesha mwanamke kuwa kama: mtoto, dada, kijana; mama, mwalimu, kiongozi, mwandani na mkarimu. Mwanamke daima anaoneshwa kuwa karibu sana na Mwenyezi Mungu. Mwanamke anaweza kusaidia mchakato wa kufunda watu udugu kwa kujikita katika: ukweli na uwazi; uaminifu; kwa kuwajengea vijana utamaduni wa kupenda haki, amani na maridhiano; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; lakini jambo la msingi ni kuwa mashuhuda na vyombo vya upendo na mshikamano wa kidugu!

Sr. Raffaella Petrini kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Toma wa Akwino, Angelicum, amekazia kwa namna ya pekee kabisa Mafundisho Jamii ya Kanisa na kwamba, wanawake wanayo nafasi na dhamana ya pekee kabisa katika mchakato wa kukuza na kudumisha maendeleo endelevu ya binadamu; kwani mwanamke amekirimia na mapaji mbali mbali yanayoweza kusaidia kufikia malengo haya. Mwanamke hana tabia ya ushindani usiokuwa na tija wala mashiko; si mtu anayejikita sana katika ukiritimba kama ilivyo kwa wanaume.

Sr. Raffaella Petrini anaendelea kufafanua kwamba,  wanawake ni watu waliojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na moyo wa kujisadaka bila ya kujibakiza, kiungo muhimu sana katika ujenzi wa udugu, mafungamano ya kijamii, kisiasa na kiuchumi duniani! Mkutano wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, umehitimishwa, Ijumaa, tarehe 9 Juni 2017 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekaza kusema kuwa majadiliano ni mchakato unaopaswa kutekelezwa kwa njia ya ushirikiano makini kati ya wanawake na wanaume kwa kukazia kwanza: dhamana na wajibu wa wanawake; majiundo makini ya udugu kwa kujenga majadiliano yanayosimikwa katika maisha ili kuheshimiana na hatimaye, kujenga urafiki katika jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.