2017-06-09 15:41:00

Papa Francisko: Mwenyezi Mungu ni kiini cha furaha na matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa, tarehe 9 Juni 2017 amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa kusali bila kuchoka wanapokabiliwa na matatizo, changamoto, shutuma na hata madhulumu katika maisha. Wajenge na kudumisha matumaini kwa Mwenyezi Mungu ambaye atawasaidia na kuwainua kwa wakati muafaka kadiri ya mapenzi yake! Kamwe wasikubali kudanganywa na mazuri ya ulimwengu huu yanayopita na kutoweka kama umande wa asubuhi na hatimaye, kubaki wakiwa watupu!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwimbia daima Mwenyezi Mungu wimbo wa furaha, matumaini na mapendo, kwani anawajalia wokovu kama ilivyojitokeza kwenye somo la kwanza kutoka kwenye Kitabu cha Tobiti 11: 5-17. Hii ni historia ya maisha ya kifamilia inayoundwa na wazazi: Tobiti aliyekuwa kipofu na mwanaye Tobia pamoja na mke wake Sara ambaye alikuwa anashutumiwa kwa kusababisha vifo vya wanaume kadhaa hapo mjini. Hii ni familia ambayo imeonja furaha, machungu, magumu na changamoto za maisha. Mke wa Tobiti alichakarika mchana kutwa ili kuhakikisha kwamba, familia yake inapata mahitaji msingi. Hawa ni watu waliojaribiwa sana katika maisha kiasi hata cha kutaka kutema zawadi ya maisha, lakini wakapata matumaini kwa Mwenyezi Mungu.

Hali kama hii, anasema Baba Mtakatifu inampata kila mtu katika safari ya maisha yake ya imani na wote wanakimbilia  katika sala kama faraja na kitulizo katika maisha yao na sala hii inakuwa ni chemchemi ya matumaini kwa ndugu zao. Sala endelevu na udumifu ni mambo msingi sana katika maisha ya waamini hasa nyakati zile ambazo watu wanakata tamaa ya maisha kutokana na shida pamoja na changamoto mbali mbali za maisha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata katika maisha kuna nyakati za furaha zinazobubujika katika maisha ya watu baada ya kuvuka majaribu makubwa na hatimaye, kuona wokovu unaoletwa na Mwenyezi Mungu. Huu ndio wakati muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, furaha na shukrani.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari moyoni mwao na kuona ni nyakati zipi ambazo wamepitia katika usiku wa giza nene kiasi hata cha kukata tamaa ya maisha! Nyakati kama hizi ni sehemu ya Msalaba wa maisha ya mwamini zinazoweza kuvukwa kwa njia ya sala endelevu na uvumilivu kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu, daima yuko pamoja na waja wake na kamwe hatawaacha wapotee kama ndoto ya mchana! Wawe wadumifu katika sala. Anawashauri waamini kujitaabisha kujisomea sehemu hii ya Maandiko Matakatifu katika maisha yao ili kuweza kutafakari safari ya maisha yao ya kiroho, ili kujipatia mwanga wa kusonga mbele katika shida na changamoto mbali mbali za maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.