2017-06-09 15:53:00

Hali tete ya Jimbo Katoliki Ahiara, Nigeria kupatiwa ufumbuzi!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 8 Juni 2017 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa familia ya Mungu kutoka Jimbo Katoliki Ahiara, Nigeria uliongozwa na Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja ambaye pia ni msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Ahiara. Ujumbe huu kutoka Jimbo Katoliki la Ahiara umefanya hija ya kitume kwa kutembelea Makanisa makuu yaliyoko Jimbo kuu la Roma pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Makanisa haya. Alhamisi asubuhi, walishiriki pia katika Ibada ya Misa Takatifu iluyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Taarifa inasema kwamba, ujumbe huu pia ulipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambao kwa pamoja wamepembua kwa kina na mapana hali ya maisha na utume wa Jimbo Katoliki la Ahiara, Nigeria ambalo tangu mwaka 2014 Askofu aliyeteuliwa kuongoza Jimbo hili hajakubaliwa na waamini kuanza kutekeleza utume wake kama kiongozi mkuu. Hii inatokana na kuwepo kwa makundi mawili, yanayopinga uteuzi wa Askofu Peter Okpaleke wa Jimbo la Ahiara na kundi jingine linalokubali uteuzi huu, hali ambayo imesababisha “kuchafuka kwa hali ya maisha na utume wa Kanisa Jimboni humo”.

Baada ya kuzungumza na kujadiliana na Baba Mtakatifu Francisko amesikitika kusema, hali kama hii haiwezi kukubalika hata kidogo na kwamba, baada ya tafakari ya kina na sala, atatoa uamuzi wake. Tangu sasa, Baba Mtakatifu anapenda kuliaminisha Jimbo Katoliki la Ahiara chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Viongozi wengine waliokuwemo kwenye msafara huu ni pamoja na Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria pamoja na Bwana Stanley Pius Iwu, mkuu wa kabila katika eneo la Ahiara.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.