2017-06-08 13:37:00

Baraza la Maaskofu Katoliki Austria jicho kodo Sinodi ya vijana


Baraza la Maaskofu Katoliki Austria (Öbk), linakutana katika mkutano wake mkuu wa mwaka kuanzia tarehe 12 – 14 Juni 2017, katika madhabahu ya kitaifa ya Bikira Maria, Mariazell, chini ya uenyekiti wa Kardinali Christoph Schönborn, ambaye ni Askofu mkuu wa Vienna. Katika mkutano wao huo, Maaskofu wa Austria wameweka kipaumbele katika maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayofanyika mjini Vatican, mwezi Oktoba 2018, ikiongozwa na kauli mbiu: Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito.

Baraza la Maaskofu Austria, litatumia muda pia kujadili suala la usalama, makanisani na katika jamii ya Austria kwa ujumla. Maaskofu wananuia kuliaminisha tena taifa lao katika tunza na maombezi ya Mama Bikira Maria. Mkutano mkuu wa Maaskofu Austria utaanza tarehe 12 Juni saa tisa alasiri kwa sala ya pamoja katika Kanisa Kuu la Marizell. Tarehe 13 Juni, Askofu mkuu Peter Stephan Zurbriggenalle, Balozi wa Vatican nchini Austria, ataongoza Misa Takatifu katika kanisa kuu la Marizell, na tarehe 14 majira ya mchana watahitimisha mkutano wao.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.