2017-06-07 14:09:00

Umuhimu wa mshikamano wa kimataifa kuboresha maisha ya binadamu


Kuna haja kubwa kutambua umuhimu wa mshikamano wa kimataifa kama sehemu ya msingi katika kushiriki na kufurahia haki msingi za binadamu wote, katika harakati za kutafuta maisha bora kwa familia ya binadamu, na katika kutetea na kulinda mafao ya wote. Askofu Mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, nchini Uswiss, katika hotuba yake kwenye kikao cha 35 cha Baraza la Haki za Binadamu, anawaalika Jumuiya ya kimataifa kutambua mshikamano wa kimataifa kama moja ya njia za thamani katika kuhangaikia haki na usawa wa utaratibu mzima wa uchumi na siasa kimataifa.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anaeleza kwamba Vatican inaamini na inaalika mataifa yote kuamini na kulifanyia kazi kwa haraka hitaji la kushikamana na kutenda kwa pamoja hasa katika kipindi hiki ambapo kuna changamoto kubwa za wahamiaji, mabadiliko ya tabia nchi, majanga asilia, machafuko na kinzani zinazoendeshwa kwa nguvu ya mtutu, na tofauti kubwa inayozidi kuonekana kati ya maskini na tajiri. Wananume na wanawake duniani kote, watambue kwamba wanadaiwa kushikamana ili kutengeneza kwa pamoja mazingira yanayofaa binadamu kuishi, kutunza na kuendeleza hazina ya urithi isiyogawanyika wala kutenganishwa, hazina inayoundwa na mfumo mzuri wa utamaduni, sayansi na teknolojia, vikiwemo viumbe vinavyoonekana na visivyoonekana.

Mshikamano sio kazi ya umma, bali kama anavyofundiha Baba Mtakatifu Francisko, mshikamano ni utendaji halisi wa kila shughuli za kisisasa, kiuchumi, kisayansi, na katika mahusiano kati ya watu binafsi, mataifa na kati ya nchi na nchi. Utamaduni wa kupotezea mambo ya msingi, utashindwa iwapo watu wataelimishwa kuwa na mshikamano wa kweli.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anaalika Umoja wa kimataifa kutohofia mshikamano, kwani mshikamano haupingani na utawala, bali unasaidia zaidi kuelewa maana ya utawala kama namna ya kujitambua na kujieleza kwa uhuru kati ya watu. Mshikamano usitazamwe kana kwamba ni wajibu tu, bali utambuliwe kuwa ni tunu ya kimaadili inayobubujika kutoka kwenye kanuni ya udugu kati ya wanadamu. Mshikamano ni uwajibikaji unaohusu kila mmoja kwa ajili ya kujali wengine, hasa walio wanyonge. Hivyo unahitajika ushiriki binafsi, taasisi, mataifa, na kimataifa ili kufikia malengo kamili ya utu wa binadamu na mafao ya wote.

Mshikamano wa kimataifa ni ushiriki wa kila mmoja katika mchakato wa kufanya maamuzi ya pamoja, na kwa namna ya pekee kutambua kanuni ya ushirikishaji wajibu. Mshikamano na Ushirikishaji au mgawanyo wa wajibu ni kanuni zinazotegemeana sana, kwani mgawanyo wa wajibu ni namna ya kusaidia mwanadamu kwa kupitia sekta mbali mbali zinazojitegemea.

Itakumbukwa kwamba mwaka 2015 viongozi wa Jumuiya ya kimataifa waliafiki kukabiliana na changamoto hatarishi zinazokabili familia ya mwanadamu, ambapo walikubaliana namna ambavyo ingependeza hali ya uchumi, siasa, jamii na mazingira ionekane kufikia mwaka 2030. katika Agenda ya 2030, Jumuiya ya kimataifa imechagua mshikamano na kutupilia mbali ubinafsi. Mshikamano na wanaotengwa, mshikamano na maskini wa leo, mshikamano na kizazi kijacho.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anasisitiza kutokomeza kabisa mizizi ya utengano, uonevu, umaskini, na ukosefu wa usawa na uwiano kati ya mataifa. Mtazamo na utendaji wa namna hii ndiyo utakaoleta amani, usalama, na maendeleo, ikiwa ni pamoja na utetezi wa haki msingi za binadamu. Katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mwezi Marchi, Baba Mtakatifu Francisko, alisema kwamba mshikamano ni kinga ya utengano mamboleo. Mshikamano ni ufahamu wa kujitambua kuwa wote ni wamoja, wakati huo huo kuwa na uwezo wa kujali na kuhangaikia wengine kwa pamoja, sababu mmoja anapoteseka, wote wanateseka, na mmoja anapokuwa na furaha wote wanakuwa na furaha.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.  

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.