2017-06-07 14:29:00

Mt. Antony wa Padua shule ya ibada kwa Maria na huduma kwa wanyonge


Tarehe 13 Juni, Kanisa linapoadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Antony wa Padua mwaka huu ambapo madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima inaadhimisha miaka 100 tangu Mama Maria awatokee watoto Lucia, Francisko na Yasinta huko Fatima, Ureno, Padre Oliviero Svanera, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mt. Antony wa Padua, anatoa ujumbe akiwaalika wote wenye ibada kwa Mt. Antony wa Padua, na waamini wote kuendeleza ibada kwa Mama Bikira Maria na kujali wanyonge.

Katika maisha yake Mt. Antony amekuwa na ibada kwa Mama Bikira Maria, akijiweka katika tunza na maombezi yake. Katika kumbukumbu za mahubiri aliyokuwa akiandika, kuna mahubiri mazuri ya siku ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni. Ikumbukwe kwamba Mt. Antony wa Padua alizaliwa Lisbon Ureno, tarehe 15 Agosti 1295. Wakati huo huo Mt. Maximilian Kolbe aliyejali na kutetea sana maskini na wanyonge, alikufa shahidi siku ya mkesha wa Sikukuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni tarehe 14 Agosti 1941, huko Auschwitz, Poland.

Mt. Antony amewahi kuandika kwamba, wakristu ni lazima watabasamu na kufurahi pamoja na Bikira Maria kwa kumwilishwa kwake Kristo Yesu kwa ajili ya wanadamu, lakini pia ni lazima kushiriki mateso yake kama alivyoshiriki Bikira Maria akimuona mwanae akiuawa msalabani. Ni katika ushiriki wa yote hayo ambapo Mama huyu alibaki kuwa mwaminifu mpaka mwisho, ndio sababu mwanae alipenda kumpaliza mbinguni.

Ni mwaliko kwa waamini wote kuvumilia kwa uaminifu taabu na mahangaiko mbali mbali ya maisha, ili siku moja waweze pia kushiriki furaha na utukufu katika jumuiya ya watakatifu mbinguni. Kama kristu alivyomnyanyua Bikira Maria katika unyonge wake na kumpa utukufu mbinguni, ndivyo atakavyowanyanyua wanyonge katika taabu zao, kama anavyoimba Mama Bikira Maria mwenyewe “amewashusha wenye nguvu toka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu” (Luka 1: 52).

Mt. Antony wa Padua alijifunza unyenyekevu wa Mama Bikira Maria, akashinda vishawishi vya madaraka, majivuno na mambo ya dunia. Hakuna huduma ya siasa, elimu, afya, kazi yeyote au maisha ya familia yatakayoweza kuwa na mafanikio bila unyenyekevu. Kama vile Kristo anavyowaosha miguu mitume, ndivyo anavyoalika kila mmoja katika huduma yeyote, kuhangaikia wengine kwa unyenyekevu na sio kuwa na majivuno (Rej. Yohane 13:12). Kwa hali ya jamii leo, ni lazima kuwahudumia na kuwahangaikia kwa namna zote wakimbizi, wahamiaji, wasio na kazi, wapweke, wagonjwa, wafungwa, maskini na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Waamini watakuwa wafuasi kweli wa Kristo wenye kuzaa matunda bora na yanayodumu, iwapo watajifunza kujitoa kwa ajili ya wengine kwa unyenyekevu kama alivyofanya Mt. Antony wa Padua, hata ikibidi kujitoa sadaka kubwa, kama alivyojitoa Mt. Maximilian Kolbe, akakubali kufa yeye ili aokoe maisha ya baba wa familia. Kwa maombezi ya Mama Bikira Maria, na watakatifu Antony wa Padua na Maximilian Kolbe, waamini wataweza kumshuhudia Kristo wa msalaba, na kuleta utukufu wa Mungu kati ya watu katika dunia hii ya leo yenye changamoto nyingi ambapo wanyonge wanaonekana kuathirika zaidi.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.