2017-06-06 14:57:00

Papa Francisko asema, unafiki ni kinyume cha Ukristo!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican siku ya Jumanne, tarehe 6 Juni 2017 amewaonya waamini kwamba, unafiki si lugha ya Kristo Yesu na kamwe haipaswi kuwa ni lugha inayotumiwa na Wakristo! Baba Mtakatifu alikuwa anafanya rejea kwenye Injili ya siku ambamo baadhi ya Mafarisayo na Maherodi walitaka kumnasa kwa kumjaribu kuhusu kulipa kodi!

Yesu akawaambia yaliyo ya Kaisari apewe Kaisari, na yaliyo ya Mungu apewe Mungu mwenyewe! Waamini wanapaswa kuwa mbali sana na chachu ya unafiki na maisha ya undumila kuwili kama walivyoonesha Mafarisayo! Ni watu waliokuwa wanazungumza na kuwahukumu wengine. Yesu aliamua kusimamia ukweli. Viongozi wa Kanisa wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wanatumbukia au kutumbukizwa katika unafiki na itakuwa ni changamoto kubwa sana kuweza kuvuka kutoka katika hali kama hiyo! Majaribu yanaanza kwa kuwa na nia mbaya, kama inavyojionesha kwenye Injili kwa Mafarisayo kuhusu kodi kwa Kaisari. Yesu akawauliza mbona walitaka kumjaribu kwa kumtega kwa swali kama lile? Yesu anaamua kujikita katika ukweli na kuwataka Kaisari atendewe kama Kaisari na Mwenyezi Mungu apewe sifa na heshima yake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, unafiki unafumbatwa katika lugha ya kudanganya watu wengine, ili hatimaye, kuwatumbukiza katika ubaya, kwa kuharibu maisha yao: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anasema, ikiwa ndani ya Jumuiya kuna wanafiki, hapo iko hatari kubwa kwa maisha ya wanajumuiya. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wajifunze kusema, na kusimamia ukweli, kwani zaidi ya hapo ni kukimbilia uvuli wa shetani. Unafiki unaharibu sana maisha na utume wa Kanisa. Waamini wawe na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia ukweli katika maisha ili kuondokana na unafiki hatari kubwa sana. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuomba neema ya kutangaza na kusimamia ukweli katika maisha, kwa kuondokana na nia mbaya inayoweza kuwatumbukiza katika unafiki, chachu hatari sana kwa ustawi na maendeleo ya Kanisa. Kama huwezi kusema, ukweli ni afadhali ukae kimya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.