2017-06-06 15:45:00

Mchango na utume wa Wakarismatiki Wakatoliki ndani ya Kanisa!


Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki Duniani limekuwa ni tukio la Uekumene wa sala, maisha ya kiroho na huduma na ushuhuda wa imani ya Kikristo inayofumbatwa katika damu! Wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wametumia maadhimisho haya kutafakari, kusali, kutubu, kuongoka na kumshukuru Mungu kwa mafuriko ya neema yaliyoliwezesha Kanisa kutambua na kutathimini mchango wa chama hiki katika maisha na utume wa Kanisa!

Padre Augustine John Temu kutoka Jimbo Katoliki la Tanga, Tanzania ni kati ya mahujaji 120 kutoka Tanzania walioshiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki Duniani. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha changamoto za kiekumene zilizopelekea hata kuanzishwa kwa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki Duniani. Umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu imani; Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.

Padre Augustine John Temu anagusia pia ulegevu wa maisha ya kiroho na mafundisho potofu yaliyopelekea baadhi ya Wanakarismatik kushindwa kutambua umuhimu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Kitubio; dhamana na nafasi ya Bikira Maria katika kazi ya ukombozi. Amekumbusha kwamba, Ekaristi Takatifu ni kiini na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa na kwamba, hakuna Kanisa wala Wakristo pasi na Ekaristi Takatifu, kwani ni Kristo Yesu mwenyewe! Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika hija ya maisha ya waamini kwa kutambua kwamba, inawawezesha tena kupata neema ya utakaso, kwa kuomba msamaha na kupata maondoleo ya dhambi.

Ni matarajio yake kwamba, waamini wengi wataendelea kujiunga na Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki iliĀ  kusoma, kulitafakari na kulifafanua Neno la Mungu kadiri ya maisha na mazingira yao, tayari kulitolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Chama hiki kina mvuto mkubwa wa maisha ya sala inayogusa undani wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Yote haya yanafanyika ili kuwaimarisha waamini katika imani, matumaini na mapendo; kwa Mungu na kwa jirani zao.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Chama hiki yamekuwa ni nafasi ya kukuza na kudumisha uekumene wa sala, maisha ya kiroho na huduma kwa kukutana na Wakristo kutoka sehemu mbai mbali za dunia. Wametambua kwamba, wao ni sehemu ya Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Wanahamasishwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika tofauti zilizopatanishwa na Roho Mtakatifu kama anavyokaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.