2017-06-05 15:17:00

Matendo ya huruma yanawawezesha waamini kushiriki mateso ya wengine!


Matendo ya huruma kiroho na kimwili ni sehemu ya mchakato unaomwezesha mwamini kushiriki katika mateso na mahangaiko ya wengine, kwa kuhatarisha maisha yake sanjari na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Jumanne tarehe 5 Juni 2017, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Kanisa linapoadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Bonifasi, Askofu, Shahidi na Mtume wa Kanisa la Ujerumani, wakati huu, Kanisa linapoanza Kipindi cha Mwaka wa Kawaida wa Kanisa.

Baba Mtakatifu amekita mahubiri yake kutoka kwenye Kitabu cha Tobiti kinachoonesha utauwa wa Tobiti, aliyewasaidia Waisraeli waliokuwa utumwani kwa sadaka na majitoleo yake kiasi hata cha kutaka kuhatarisha maisha yake! Alijitahidi kuwazika ndugu zake kwa heshima kuu; akakumbana na mkono wa chuma kiasi cha kunyang’anywa mali na utajiri wake wote. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutafakari kwa kina na mapana matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama ushuhuda wa kushiriki mateso na mahangaiko ya wengine, kwa kujibu kilio chao kwa mwanga na matumaini ya Injili.

Jambo la msingi ni kwa waamini kuchunguza dhamiri zao ili kuona ikiwa kama kweli wamekuwa ni wakarimu, wanaoweza kusikiliza na kujibu shida na mahangaiko ya jirani zao. Kutekeleza na kumwilisha matendo ya huruma kuna changamoto zake, kiasi hata cha kuhatarisha maisha, kama ilivyotokea mjini Roma! Kuna umati mkubwa wa watu waliothubutu kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kuwalinda Wayahudi wasipelekwe kwenye kambi za mateso na mauaji ya kinyama, kama alivyofanya Papa Pio XII! Alijitahidi kuwalinda, kuwaficha na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ili wasitekwe na kupelekwa kwenye kambi za mateso na mauaji! Papa Pio XII akahatarisha sana maisha yake, lakini akathubutu kumwilisha matendo ya huruma, ili kuokoa Injili ya uhai.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, hata wakati mwingine wale wanaotenda matendo ya huruma wanaweza kubezwa na kudhihakiwa na wengine, kama ilivyojitokeza kwa Tobiti aliyekuwa anathubutu kuacha mambo mengine yote ili aweze kwenda kuwazika ndugu zake; kuwalisha na kuwanywesha maskini. Hii ndiyo changamoto inayotolewa kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajisadaka na kujitoa kimasomaso kwa ajili ya kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wale wanaohitaji zaidi msaada wao. Huduma inayofumbata sadaka na majitoleo, kama ilivyojitokeza kwa Kristo Yesu, akadiri kufanya Njia ya Msalaba na hatimaye, kuinama kichwa na kutoa roho pale Msalabani, ili kumwonjesha binadamu huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Waamini wajifunze kumwilisha matendo ya huruma katika maisha yao kwa kutambua kwamba, hata wao wamehurumia na kupendwa kwanza na Mwenyezi Mungu. Amewahurumia na kuwasamehe dhambi na makosa yao, changamoto kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa jirani zao. Matendo ya huruma, yanawasaidia waamini kuondokana na ubinafsi, tayari kuiga na kumfuasa Kristo kwa ukaribu zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.