2017-06-05 07:53:00

Majadiliano ya kiekumene yanapaswa kujikita katika ushuhuda wa pamoja!


Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka kwa Makanisa yote ya Kikristo kwa Mwaka 2017 imekuwa ni fursa muhimu sana ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene hasa kwa kuzingatia uekumene unaofumbatwa katika sala na maisha ya kiroho; uekumene unaoshuhudiwa katika damu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama ushuhuda wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa watu wa mataifa! Roho Mtakatifu ni mhusika mkuu katika kuwaunda na kuwafunda wafuasi wa Kristo ndani ya Kanisa, kumbe, Wakristo hawana budi kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwafunda barabara, ili kweli waweze kuwa ni chachu ya mabadiliko katika ulimwengu mamboleo.

Haya ndiyo yaliyofikiwa hivi karibuni katika mkutano wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Wawakilishi wa Makanisa ya Kipentekosti (Joint Consultive Group, Jcg) uliohitimishwa hivi karibuni huko California nchini Marekani katika mkutano wake wa awamu ya tatu baada ya kutimia takribani miaka ishirini tangu ule mkutano wa kwanza uliponyika Harare nchini Zimbabwe kunako mwaka 1998. Huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Makanisa ya Kipentekosti, ili kuweza kufikia maamuzi ya pamoja katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Lengo ni kushirikishana uzoefu na mang’amuzi ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwa na mbinu mkakati wa kimissionari baina ya Makanisa ya Kikristo, ili kutangaza na kushuhudia kwa pamoja tunu msingi za Kiinjili. Mambo haya yakajadiliwa tena katika mkutano baina ya wawakilishi wa Makanisa ya Kipentekosti na Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mkutano uliofanyika huko Porto Alegre na hatimaye, kufikia uamuzi wa kuwa na usomaji wa pamoja wa Maandiko Matakatifu. Mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni uliofanyika huko Busan, Korea ya Kusini kunako mwaka 2013 ukakazia umuhimu wa utekelezaji wa maamuzi msingi yaliyofikiwa kwenye mikutano iliyotangulia hapo awali.

Mkazo ukawa ni umuhimu wa kuwafunda waamini katika uelewa wa Maandiko Matakatifu kwa kuzungatia na kuheshimu Mapokeo ya Kikristo, huku Roho Mtakatifu akipewa kipaumbele cha kwanza katika kuwafunda waamini Habari Njema ya Wokovu, tayari kwenda kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kati ya watu wa Mataifa. Kumbe, majadiliano ya kiekuemene yanapaswa pia kujikita katika ushuhuda wa pamoja ambao kimsingi ni matunda na kazi ya Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa.

Utamaduni wa upendo, mshikamano, ukarimu sanjari na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha ni kati ya mambo msingi ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga na wakristo wote sehemu mbali mbali za dunia kama ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika huduma. Kuna haja pia ya kuendeleza uekumene wa sala kwa kushirikiana na Wakristo wa Makanisa mbali mbali, ili kumpatia nafasi ya pekee Kristo Yesu katika maisha na vipaumbele vyao. Wakristo watambue kwamba, Yesu ni Mkombozi wa wote anayewahamasisha kushikimana katika umoja, udugu, sala na huduma.

Jiji la Arusha, Tanzania linatarajiwa kuwa ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa Makanisa ya Kipentekosti duniani (World Mission Conference) utakaoadhimishwa kunako mwaka 2018! Hapa wajumbe watazama zaidi ili kupembua juu ya “Wito wa Roho Mtakatifu na ushuhuda wa Kikristo”. Makanisa ya Kipentekosti pamoja na Baraza la Makanisa Ulimwenguni yanaendelea kujizatiti zaidi katika kuondokana na mawazo mgando ambayo kwa sasa yamepitwa na wakati kwa kutambua dhamana na mchango wa Makanisa ya Kipentekosti katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Wakristo wanahamasishwa kujikita zaidi katika mambo msingi yanayowaunganisha zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.