2017-06-04 14:36:00

Sala ya Kanisa kwa ajili ya mahitaji ya familia ya Mungu!


Ibada ya Misa takatifu imehudhuriwa na umati mkubwa wa waamini kutoka ndani na nje ya Italia. Wakati wa Sala ya Waamini, Kanisa limekumbukwa na kuombewa mapaji ya Roho Mtakatifu ili liweze kujenga na kudumisha imani na mapendo. Limewaombea viongozi wakuu wa nchi ili Roho Mtakatifu aweze kuwaongoza katika kutafuta na kudumisha misingi ya haki na amani ya kweli. Katika shida na mahangaiko ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, waamini wamesali kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoa wale wanaowanyanyasa na kuwadhulumu wengine, ili hatimaye, waweze kumtambua Yesu kuwa ni Bwana.

Kanisa limewaombea vijana wa kizazi kipya, ili waweze kujisadaka kwa ajili ya maisha na wito wa Kipadre. Ombi kwa lugha ya Kiswahili limetolewa na Sr. Selela Alfonce Lucas wa Shirika la Kuabudu Moyo Mtakatifu wa Yesu aliyemwomba Mwenyezi Mungu kukaa kati ya watu wake kwa njia ya Roho Mtakatifu, ili awafundishe kusali na kuishi katika utii asili wa Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.