2017-06-04 14:05:00

Roho Mtakatifu ni kiungo cha umoja wa Wakristo katika utofauti wao!


Sherehe ya Pentekoste, yaani Siku 50 baada ya Ufufuko wa Kristo Yesu, Kanisa linahitimisha Kipindi cha Pasaka kwa kupokea Zawadi ya Roho Mtakatifu; Roho Muumbaji anayefanya yote kuwa mapya katika maisha na utume wa Kanisa; mapya haya yanajitokeza katika wanafunzi wanaofanywa upya kwa kuwa na moyo mpya! Hawa ni watu wapya walioumbwa na kushukiwa na Roho Mtakatifu, akawajalia mapaji ya kuweza kuzungumza lugha mbali mbali, lakini wote wakiwa wameunganishwa katika kifungo cha umoja. Hiki ni kielelezo cha utofauti katika umoja, unaofumbatwa katika Kanisa la Kiulimwengu.

Daima katika nyakati mbali mbali kumekuwepo na karama na mapaji ambayo Roho Mtakatifu amelikirimia Kanisa lake. Ni Roho Mtakatifu anayeratibu mchakato mzima wa umoja, ili kuwaunganisha wote katika roho moja, hata kama wako tofauti kiasi gani! Kwa njia hii umoja wa kweli unaweza kupatikana kadiri ya mapenzi ya Mungu na wala si kufanana, bali ujenzi wa umoja katika tofauti! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye maadhimisho ya Siku kuu ya Pentekoste, Jumapili tarehe 4 Juni 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican! Uwanja uliofurika na umati mkubwa wa waamini kutoka ndani na nje ya Italia, wengi wao wakiwa ni wanachama wa Chama cha Wakarisimatiki Wakatoliki wanaohitimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama chao!

Baba Mtakatifu ameonya kwamba, kuna vishawishi vikuu viwili ambavyo vinapaswa kuepukwa katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa! Jambo la kwanza ni kutafuta utofauti bila ya kuwa na umoja na jambo la pili ni kutafuta umoja bila ya kuwa na utofauti! Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kishawishi cha kwanza ni pale ambapo watu wanataka kutenganisha kwa kujiamria mahali pa kushikamana kwa kuwa na misimamo mikali na utendaji wake, kiasi cha kudhani kwamba, wao ni bora zaidi kuliko hata wengine, hapa kinachochukuliwa ni sehemu ndogo kwa kuacha sehemu kubwa ya Kanisa. Watu wanashikamana kwa makundi, badala ya kujisikia kuwa ni wamoja katika Roho Mtakatifu. Matokeo yake ni kuwa ni Wakristo wa mlengo wa kulia na Wakristo wa mlengo wa kushoto, badala ya kuwa ni Wakristo wa Yesu mwenyewe. Matokeo yake ni utofauti pasi na umoja!

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza kwa kusema, kishawishi cha pili ni kutafuta umoja pasi na utofauti, kwani hapa umoja unageuzwa kuwa ni kufanana na kwamba, kila mtu anapaswa kufiriki na kutenda kama wengine pasi na tofauti na matokeo yake, umoja unatoweka na kubaki watu kufanana kwa namna moja na hapa uhuru ambayo kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu unatoweka. Baba Mtakatifu anasema, sala ya waamini hapa ni kuomba neema ya Roho Mtakatifu ili kuweza kupokea umoja unaokumbatia na kupenda licha ya tofauti ya matamanio binafsi, Makanisa na Madhehebu, bali umoja kwa wote kwa kuondokana na “udaku” unaotaka kupandikiza magugu, chuki na uhasama kati ya Wakristo, ili kujenga na kudumisha umoja katika roho, ili kweli Kanisa liweze kuwa kuwa ni chombo cha ukarimu, wazi na mahali pa kushirikishana furaha ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake anakaza kusema upya unaoletwa na Roho Mtakatifu ni moyo mmoja, zawadi ya Roho Mtakatifu anayewapatia Mitume wake mamlaka ya kuondoa na kusamehe dhambi pasi na kuhukumu ingawa baadhi yao walimsaliti na kumkana wakati wa mateso na kifo chake Msalabani.  Ikumbukwe kwamba, Roho Mtakatifu ni zawadi ya kwanza kutoka kwa Kristo Mfufuka aliyowakirimia Mitume wake, ili kuwapatia uwezo wa kuwaondolea watu dhambi zao! Kumbe msamaha wa dhambi ndio mwanzo wa uwepo wa Kanisa, kwani msamaha ni nguvu ya upendo unaowaunganisha na kuwaimarisha watu katika umoja bila kuteteleka hata kidogo. Msamaha unauweka huru moyo wa mwamini ili kuanza upya; msamaha ni chemchemi ya matumaini na pasi na msamaha, haiwezekani kujenga Kanisa.

Roho wa Msamaha anawezesha yote kuwa na utulivu kwa kuondokana na njia zile ambazo zinapenda kuhukumu; kufunga malango; kuwashambulia wengine. Roho Mtakatifu anawahamasisha Wakristo kutoa na kupokea msamaha; kupokea na kuambata huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma kwa jirani lakini zaidi mchakato mzima wa mageuzi unafumbatwa katika upendo! Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Roho Mtakatifu neema ya kulipyaisha Kanisa kwa njia ya msamaha; kujisahihisha wenyewe na kwa njia hii, wanaweza kupata ujasiri wa kuwasahihisha wengine katika upendo!

Waamini wamwombe Roho Mtakatifu, moto wa upendo ili uweze kuwaka ndani yao na ndani ya Kanisa, hata kama wakati mwingine, wanauzimisha moto huu kwa majivu ya dhambi zao. Roho Mtakatifu ndiye anayelitegemeza Kanisa katika umoja na utofauti wake. Waamini wana kiu ya Roho Mtakatifu, ili aweze kuwashukia na kuwafundisha umoja, kwa kupyaisha nyoyo zao pamoja na kuwafundisha kupenda kama anavyopenda yeye mwenyewe; kusamehe kama anavyowasamehe mwenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.