2017-06-04 14:51:00

Papa Francisko asema, utume ni kiini cha imani ya Kikristo!


Mara baada ya maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, Tarehe 4 Juni 2017, Baba Mtakatifu Francisko amesema,  amechapisha ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani kwa Mwaka 2017 itakayoongozwa na kauli mbiu “Utume ni kiini cha imani ya Kikristo”. Anamwomba Roho Mtakatifu kuenzi utume wa Kanisa ulimwenguni kote kwa kuwakirimia wamissionari wote nguvu ya Injili. Roho Mtakatifu anawajalie amani, agange na kuponya madonda ya vita na vitendo vya kigaidi, kama ilivyojitokeza usiku wa kuamkia Jumapili, tarehe 4 Juni 2017 huko London, Uingereza, kwa kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu Francisko amependa kuchukua fursa hii, kutoa salam zake za pekee kwa mahujaji kutoka ndani na nje ya Italia, hasa kwa namna ya pekee kabisa wanachama wa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki Duniani wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chama chao. Amewakumbuka na kuwapongeza Wakristo kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo walioungana naye katika Sala ya Malkia wa Mbingu. Mwishoni, amewaweka waamini na mahujaji wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwaombea kwa Roho Mtakatifu, wawe kweli ni mashuhuda wa ukweli wa Kiinjili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.