2017-06-04 15:37:00

Mkesha wa kiekumene umekuwa ni muda wa sala, tafakari, toba na sherehe


Mkesha wa Kiekumene wa Pentekoste kwa Mwaka 2017 limekuwa ni tukio la neema, baraka na shukrani kwa Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kujizatiti zaidi na zaidi katika kujenga na kudumisha umoja, upendo, udugu na urafiki, ili kuvuka ile dhambi ya utengano kati ya Wakristo!  Takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya watu nusu milioni wameshiriki katika mkesha huu, matendo makuu ya Mungu! Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa mkesha wa kiekumene kama sehemu pia ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Wakarisimatiki Wakatoliki Duniani, matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu, ameungana na viongozi wakuu wa chama hiki pamoja na viongozi wawakilishi wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo kukiri kwa pamoja kwamba, Kristo Yesu ni Bwana.

Hili ni tukio ambalo limejikita katika sala, tafakari na shuhuda mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa mintarafu Roho Mtakatifu. Mchungaji Giovanni Traettino wa Kanisa la Kiinjili la Upatanisho, amemkaribisha na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwaalika kushiriki katika mkesha wa kiekumene, kielelezo makini cha neema na nguvu ya Roho Mtakatifu anayeendelea kuliongoza Kanisa, ili siku moja liweze kuwa na umoja kamili. Maadhimisho haya yameratibiwa kwa namna ya pekee na Michelle Moran na Gilberto Barbosa.

Wakati huo huo, Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa amekazia sana kuhusu dhamana na wajibu wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa; toba na wongofu wa ndani; kwa kuambata nguvu ya Mungu inayookoa na kuponya; kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha sanjari na kutoa kipaumbele cha kwanza cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Utengano miongoni mwa Wakristo unapata chimbuko lake katika kiburi cha kutaka kujijengea jina na kuonekana kuwa bora zaidi kuliko wengine! Kumbe, Roho Mtakatifu ni asili ya umoja, udugu na upendo, changamoto na mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia matendo ya makuu ya Mungu katika maisha ya waja wake.

Padre Raniero Cantalamessa anasema, umoja miongoni mwa Wakristo ni changamoto endelevu kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa agizo la Kristo Yesu kwa wafuasi wake, ili wote wawe wamoja, dunia ipate kuamini! Wakristo wote ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, wanaopaswa kujikita katika ukweli na upendo; katika huduma na ushuhuda kama nyenzo msingi za uinjilishaji mpya. Wakristo wanapaswa kutambua kwamba, wao wanaunganishwa na imani moja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani: Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu; na kwamba, Yesu ni Bwana; Ni Mungu kweli na Mtu kweli aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye Umungu mmoja sawa na Baba! Wakristo wana amini katika maisha ya uzima wa milele.

Wakristo wanaunganishwa pia katika mateso na ushuhuda wa imani, ambao Baba Mtakatifu anapenda kuuita uekumene wa damu! Ili kuendelea kujikita katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, waamini wanahamasishwa kumwilisha ndani mwao, utenzi wa upendo kama ulivyotungwa na Mtume Paulo (1 Cor. 13: 4). Sherehe ya Pentekoste, ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kristo kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika mchakato mzima wa uinjilishaji. Huu ni wakati wa kuonesha na kushuhudia ujasiri katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa upande wake, Dr. Salvatore Martinez, amewashukuru wanachama pamoja na viongozi wote walioitikiamwaliko wa kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chama hiki, furaha yake ni furaha ya Kanisa zima, ambayo ilianza kuchipua kwa namna ya pekee kunako mwaka 1998, kwa kukutana na kusali pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II! Tangu wakati huo, umoja miongoni mwa Wakarisimatiki Wakatoliki umeendelea kukua na kupanuka kati ya Makanisa, Madhehebu ya Kikristo nahata katika Kanisa Katoliki, kwani hiki ni chama ambacho kwa miaka mingi, kimekuwa kikiangaliwa kwa “jicho la kengeza” hali ambayo imewafanya baadhi ya waamini kujisikia kutengwa hata ndani ya Kanisa lenyewe! Changamoto kwa wakati huu ni kusonga mbele katika kushuhudia umoja na utofauti katika maisha na utume wa Kanisa.

Baadhi ya Makardinali walioshiriki ni pamoja na Kardinali Kevin Joseph Farrel, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha; Kardinali Augustino Vallini, Kardinali Christoph Schoenborn pamoja na Kardinali Marc Ouellet. Kumekuwepo na idadi kubwa ya Maaskofu, Mapadre pamoja na viongozi wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo, bila kusahau umati mkubwa wa Wakristo na watu wenye mapenzi mema waliohudhuria tukio hili la kihistoria! Washiriki wa mkesha huu wa kiekumene, kwa pamoja wamesali sala ya kuomba msamaha kutokana na utengano ndani ya Kanisa! Wamekazia Ubatizo katika Roho Mtakatifu, anayewasukuma na kuwahamasisha kushikamana ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni Bwana na Mkombozi wa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.