2017-06-04 15:09:00

Mkesha wa kiekumene, ushuhuda wa nguvu ya Roho Mtakatifu Kanisani!


Yesu kabla ya kupaa kwenda mbinguni kwa Baba yake wa milele, aliwaagiza Mitume wake wasitoke Yerusalemu, bali waiongoje ahadi ya Baba, itakayowawezesha kubatiza si tena kwa maji, bali kwa Roho Mtakatifu. Hata ilipotimia siku ya Pentekoste wote walikuwako mahali pamoja, kukaja ghafla toka mbinguni uvumi kama uvuvi wa pepo wa nguvu ukienda kasi, wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka!

Hii ndiyo jeuri iliyowakutanisha Wakristo wa Makanisa na madhehebu kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika mkesha Kiekumene wa Siku kuu ya Pentekoste sanjari na kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Wakarisimatiki Wakatoliki Duniani, kwenye Uwanja wa “Circo Massimo” mjini Roma, kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko.  Kama ilivyokuwa kwenye Chumba cha juu, Wakristo wakiwa na nyoyo wazi, tayari kusubiri ahadi ya Baba wamethubutu kutangaza na kukiri kwamba,  “Kweli Yesu ni Bwana”.

Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakiongozwa na Roho Mtakatifu wamekusanyika ili kushuhudia umoja, udugu na mshikamano, tayari kuendeleza mchakato wa uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwamba, amani inawezekana duniani, ikiwa kama wao wenyewe ni vyombo na mashuhuda wa amani, vinginevyo hii ndoto ya mchana anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Amani kutoka kwa Kristo Yesu inawezekana kuwafikia watu wote kwa njia ya ushuhuda wa uinjilishaji, hata katika utofauti wao, lakini bado wanapatanishwa, huo ndio utofauti uliopatanishwa!

Ujio wa Roho Mtakatifu uwawezeshe kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji, wanaoweza kuzungumza kwa lugha moja, karama ya Roho Mtakatifu inayowawezesha kufahamu ujumbe wa Kristo Mfufuka! Wanachama wa Chama cha Wakarisimatiki Wakatoliki Duniani kutoka katika nchi 120 wamekutanika ili kumwimbia Roho Mtakatifu utenzi wa sifa na shukrani, kwa Jubilei ya Miaka 50 ya Chama hiki cha kitume, kilichoibuliwa kutokana na changamoto za kiekumene chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kujisomea kazi zilizoandikwa na Kardinali Suenens.

Roho Mtakatifu anawajalia waamini ujasiri wa kutoka kifua mbele, ili kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kama alivyofanya Mtakatifu Petro siku ile ya Pentekoste, lakini kabla ya hapo hakuthubutu hata kidogo, kiasi hata cha kumkana Yesu mara tatu! Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kikristo, inayowahamasisha kujenga na kudumisha umoja, upendo, udugu na mshikamano wa dhati. Jumuiya  ya kwanza ya Wakristo ikakua na kuongezeka maradufu; kwani Roho Mtakatifu anawahamasisha Wakristo wote kutoka kifua mbele ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wa wote.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha Wakristo kwamba, Uwanja wa “Circo Massimo” wakati ule wa madhulumu ya Wakristo ulitumikwa kwa ajili ya kuwatesa Wakristo ili kuwafurahisha wakazi wa Roma. Lakini leo hii, kuna mashuhuda wa imani wengi zaidi pengine kuliko hata ilivyokuwa kwenye Karne ya kwanza! Huu ndio uekumene wa damu unaoshuhudiwa na Wakristo wote! Ni wakati kwa Wakristo kushikamana katika Ibada, zawadi na kazi ya Roho Mtakatifu, ili kupendana na kushikamana, huku wakiandamana katika umoja!

Baba Mtakatifu anasema, uwepo wa Chama cha Wakarisimatiki Wakatoliki Duniani ni matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu, mafuriko ya neema kwa ajili ya utume wa Kanisa. Kumekuwepo na changamoto nyingi katika maisha na utume wa Chama hiki, lakini kwa wakati huu, kuna haja ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi, kwa kumshukuru Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kuzaliwa, kukua na kukomaa; Kanisa linapata watoto wapya kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, changamoto na mwaliko wa kuendeleza toba na wongofu wa ndani; ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua nafasi hii, kuwashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka ili kuhakikisha kwamba, chama hiki kinafikia ukomavu wake.Jubilei ni kipindi cha kuserebuka, tayari kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Chama hiki ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu, kwani wanachama wake wamebatizwa katika Roho Mtakatifu, kwa jili ya kumtolea Mungu sala inayomwilishwa katika huduma; kipimo atakachotumia Kristo Yesu, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza kwa namna ya pekee kabisa, Udugu wa Kikatoliki na Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki Kimataifa. Anakazia umuhimu wa kuwa na Katiba moja inayokuza umoja na udugu. Anawashukuru kwa uaminifu wao kwa Neno la Mungu; ushuhuda katika huduma, toba na wongofu wa ndani, tayari kudumisha uekumene wa sala, maisha ya kiroho, huduma na damu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.