2017-06-03 17:12:00

Utume ni kiini cha imani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa!


Utume ni kiini cha imani ya Kikristo ndiyo kauli mbiu iliyokuwa inaongoza mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa uliofunguliwa tarehe 29 Mei 2017 na kuhitimishwa Jumamosi, tarehe 3 Juni 2017 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Mkutano huu umekuwa ni wakati wa sala na tafakari ya kina; umoja na mshikamano wa kidugu, kwa ajili ya kujizatiti katika huduma ya kitume. Imekuwa ni wakati muafaka wa kusali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu Francisko, kwani wanatambua kwamba, wao ni wadau wakuu katika utekelezaji wa dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Haya yamesemwa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, wakati alipokuwa anamkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuweza kuzungumza na  na wajumbe wa mkutano huu, kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau, hata wao kwa njia ya Neno la Mungu na maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu; wanataka kuambata mchakato wa wongofu wa ndani, ili kushuhudia imani inayowashirikisha watu wengi zaidi katika maisha na Fumbo la Pasaka ya Kristo. Utume huu unabubujika kutoka katika imani kwa Kristo na Kanisa lake; imani inayofumbatwa katika upendo wenye huruma, sanjari na kutambua kwamba, Injili ya Kristo ni changamoto endelevu kwani hadi sasa hakuna Jumuiya ya Kikristo inayoweza kujidai kwamba, imekamilika, kumbe bado kuna haja ya kuendelea kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko anasema, Kardinali Filoni.

Utume ni kiini cha imani inayobubujika kutoka katika upendo unaookoa ambao kamwe hauna kikomo! Kanisa linahitaji kupyaishwa daima kutoka katika undani wake, kwani kila mtoto wa Kanisa anahitaji kufanya toba na wongofu wa ndani; anahitaji wokovu. Kwa moyo unaowaka mapendo, daima utaendelea kupenda, kutangaza, kushuhudia na kuhudumia. Mwishoni, Kardinali Filoni amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kukubali kukutana nao pamoja na kuwapatia changamoto za kufanyia kazi katika mchakato mzima wa maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.