2017-06-03 17:36:00

Roho Mtakatifu awasaidie Wakristo kujenga na kudumisha umoja!


Baba Mtakatifu Francisko anapongeza na kuwashukuru wanachama wa Chama cha Wakarisimatiki Wakatoliki au kama kinavyojulikana na wengine Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Duniani, wanaoendelea kujipambanua kwa njia ya majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika sala na huduma! Kabla ya mkesha wa maadhimisho ya Siku kuu ya Pentekoste, yanayofanyika kwenye Uwanja wa “Circo Massimo” mjini Roma, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 3 Juni 2017 amepata nafasi ya kukutana na kusalimiana walau kwa ufupi na viongozi wa Makanisa na Madhehebu ya Kikristo waliofika mjini Roma, kwa ajili ya kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chama hiki cha kitume!

Baba Mtakatifu amewaomba viongozi wote hawa kujizatiti kikamilifu katika kujenga na kudumisha umoja wa Wakristo duniani, kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwafundisha, kuwaongoza na kuwakumbusha mambo  msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Roho Mtakatifu anajenga na kudumisha umoja pale palipo na utengano. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kufanya hija ya pamoja katika sala, maisha ya kiroho, ushuhuda na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anasema, hii ni huduma ya upendo inayoweza kumwilishwa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi. Wakati wakristo wakiendelea kuchakarika katika ushuhuda, wanataalimungu nao waendelee kujizatiti kuwasaidia waamini kutambua kasoro zilizopo, ili kuzimaliza tayari kuwa wamoja katika Kristo Mchungaji mkuu!

Kardinali Odilo Scherer, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la San Paolo, Brazil anasema,  Chama cha Wakarisimatiki Wakatoliki Duniani katika kipindi cha miaka 50 kimesaidia sana kuleta mwamko wa Neno la Mungu; ushuhuda wa huduma na imani inayomwilishwa katika uhalisia wa Kanisa. Ni chama ambacho kimewawezesha waamini kutambua karama za Roho Mtakatifu na kuanza kuzifanyia kazi ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa; kwa kukamilishana katika tofauti zinazoweza kujitokeza. Katika kipindi cha Miaka 50, Kanisa limejitahidi kuwasaidia wanachama hawa kutambua sheria, kanuni na mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Kimsingi, Wana karisimatiki  Wakatoliki wamefundwa sana na Kanisa sasa ni wajibu wao kutoa ushuhuda wa imani tendaji inayojikita katika ujenzi wa Kanisa: moja, takatifu, katoliki na la mitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.