2017-06-02 16:39:00

Papa Francisko anakazia majiundo makini ya Mapadre!


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia majiundo awali na endelevu ya wakleri ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo na huruma kwa familia ya Mungu. Anakazia umuhimu wa maisha ya sala kwa mapadre vijana, ili waweze kuchota nguvu ya kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara katika maisha na utume wa Kanisa. Wawe ni viongozi wanaojitaabisha kusoma Neno la Mungu, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha katika uhalisia wa maisha na utume wao.

Maaskofu wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuhakikisha kwamba, wanakuwa karibu sana na Mapadre wao vijana hasa wanapoanza maisha na utume wao. Mapadre wawe ni watu wa sala, wanaotembea pamoja katika umoja, upendo na mshikamano, ili kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa, daima wakijitahidi kujitakatifuza kwa njia ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Mapadre vijana waoneshe kipaji cha ubunifu katika mchakato mzima wa uinjilishaji kwa kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano!

Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri  katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, malezi na majiundo ya kipadre yanapaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Jumuiya ya Wakristo inapaswa kutambua kwamba, ni sehemu muhimu sana ya majiundo na malezi ya kipadre. Mapadre watambue kwamba, wanaishi katika ulimwengu ambao ni sawa na tambara bovu linalogubikwa kwa ubinafsi, uchoyo, ukanimungu pamoja na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri kwa mwaka 2017 limekazia mambo msingi yanayofumbatwa katika Mwongozo wa Malezi ya Kipadre wa Mwaka 2016. Sifa za jandokasisi anayetamani kuwa Padre; Majiundo awali na endelevu. Kanisa linahitaji Mapadre wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa! Mapadre wanaoandamana na familia ya Mungu; wenye uwezo wa kusikiliza na kujibu kilio cha watu wao kadiri ya mwanga wa Injili. Wanapaswa kuwa ni wachungaji wema; mashuhuda makini wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; watu wakarimu, wapole na wanyofu wa moyo! Malezi na majiundo ya Kipadre yanatendeka kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya Kipadre yenye mvuto na mashiko!

Kardinali Beniamino Stella, anawakumbusha Maaskofu wa Makanisa mahalia pamoja na walezi waliopewa dhamana ya kufundisha na kuwaongoza majandokasisi katika maisha na wito wa kipadre kuhakikisha kwamba, wanaitekeleza dhamana hii kwa ari na moyo mkuu! Wawe makini katika kuchagua vijana wanaoonesha nia ya kutaka kuwa Mapadre; wawasindikize katika hija ya malezi na majiundo yao: kiakili, kielimu, kiutu, kichungaji na katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko yuko makini sana kwa malezi na majiundo ya Mapadre vijana! Anawasikiliza, anawaangalia kwa jicho na upendo wa kibaba; anaonesha matumaini makubwa katika maisha na utume wao kama jeuri ya Kanisa! Anawataka kuwa ni watu wa: Ibada na uchaji wa Mungu; viongozi wanaothubutu kutumia vyema karama na mapaji yao kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa hususan katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaodai matumizi sahihi na muafaka ya maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Watambue na kukumbuka kwamba, Kristo Yesu ndiye mlezi mkuu anayewafunda watoto wake, kwa kusaidiwa na Maaskofu pamoja na wadau mbali mbali.

Kipindi cha malezi ni wakati muafaka kwa majandokasisi kujiaminisha kwa Kristo Yesu, kwa kujenga na kudumisha uhusiano wa dhati katika Sala, Tafakari ya Neno na katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Ni wakati muafaka kwa toba na wongofu endelevu, ili kuendana na maisha ya Kristo mwenyewe; Kuhani mkuu na mchungaji mwema. Baba Mtakatifu ana matumaini makubwa kwa mapadre vijana katika maisha na utume wao, anawataka kamwe wasimwangushe Kristo kwa kumezwa na malimwengu! Neno la Mungu liwe ni shule tosha kabisa kwa mapadre vijana katika maisha na utume wao!

Itakumbukwa kwamba, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, hapo tarehe 8 Desemba 2016 limechapisha Mwongozo wa Malezi ya Kipadre  unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis”  yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Unaokazia umuhumu wa malezi na majiundo ya kipadre yanayopaswa kuboreshwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Hizi ndizo sababu msingi ambazo zimepelekea kuchapishwa kwa Mwongozo wa Malezi ya Kipadre yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” baada ya miaka arobaini na sita, tangu mwongozo wa mwisho ulipotolewa na Mama Kanisa. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee.

Kardinali Stella anasema, kunako mwaka 1970 kulitolewa Mwongozo wa Malezi ya Kipadre na kufanyiwa marekebisho kunako mwaka 1985, lakini tangu wakati huo, kumekuwepo na mageuzi na mabadiliko makubwa mintarafu historia ya watu, mahusiano ya kijamii, kitamaduni na kikanisa; maeneo ambayo Kasisi anapaswa kumwilisha maisha na utume wake wa Kipadre kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Katika kipindi chote hiki, utambulisho wa Padre umekumbana na changamoto na mabadiliko makubwa katika akili na nyoyo za watu. Kumekuwepo na mabadiliko, kiu na hamu ya watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kipadre.

Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo linakabiliana na changamoto nyingi kati yake ni Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Miaka ya hivi karibuni anaendelea kusema Kardinali Stella imeshuhudia mabadiliko makubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Kutokana na changamoto zote hizi, Kanisa limeona kwamba, kuna busara ya kuanzisha, kupyaisha na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na majiundo ya Kipadre katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekuwa ni changamoto kubwa ya kuangalia tena mchakato wa malezi na majiundo ya maisha, wito na utume wa Kipadre ndani ya Kanisa kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mapadre si watu wa mshahara, bali ni wachungaji wa familia ya Mungu, wanaopaswa kwa namna ya pekee kuwa ni watu wasikivu, wenye huruma na upendo kama ilivyokuwa kwa Kristo katika maisha na utume wake. Aliwaonea watu hurum, akawasikiliza kwa makini, akawaganga na kuwaponya, akawasamehe dhambi zao na kuwapatia tena furaha ya kuendelea kuishi kwa imani na matumaini, kwani walikuwa wameonja na kukutana na Uso wa huruma ya Mungu katika safari ya maisha yao!

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akiwaonya Wakleri kuhusu kishawishi cha kumezwa na malimwengu kwa kuwa na uchu wa mali na madaraka kwani matokeo yake ni hatari katika maisha na utume wa Kipadre. Kwa bahati mbaya, kumejitokeza katika maisha na utume wa Kipadre kwa baadhi yao kutafuta utukufu binafsi; kuwa na shingo ngumu katika shughuli za kichungaji kwa kukazia sheria peke yake bila kuonesha chembe ya huruma na mapendo kwa watu wanaotubu na kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao!

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ilikuwa ni changamoto kwa Wakleri kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Kumbe, majiundo na malezi makini ya Kipadre ni kiini cha maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, ili kweli Kanisa liweze kuwapata Mapadre wema, watakatifu na wachapakazi wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Maaskofu wanawajibika sana katika malezi na majiundo ya Majandokasisi pamoja na Wakleri wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo!

Kardinali Stella anasema, upya unaojitokeza katika Mwongozo wa Malezi ya Kipadre ni mwendelezo wa Mapokeo ya Kanisa ambayo kimsingi ni sawa na chanda na pete, kamwe hayawezi kutenganishwa, kwani Roho Mtakatifu anaendelea kuliongoza Kanisa na kulipatia fursa ya kuwa na matumaini kwa siku za usoni. Mambo msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre yamezingatiwa, yamepyaishwa na mambo mapya yameongezwa ikilinganishwa na Mwongozo wa “Pastores Dabo vobis” uliotolewa kunako mwaka 1992. Hapa mkazo ni kuwa na muungano kamili na endelevu wa majiundo na malezi ya Kipadre: kiutu, kiroho, kiakili na katika shughuli za kichungaji.

Malezi ya kiutu yanamtaka Jandokasisi kuwa na ukomavu na uwiano mzuri kati ya maisha ya kiroho na kiutu; mahusiano kati ya watu yanayojikita katika heshima na nidhamu. Bila ya kuwa na jicho la kichungaji, matatizo na changamoto zinazoweza kujitokeza katika maisha ya majandokasisi, yanaweza kuwa ni mzigo mkubwa kwaa siku za baadaye kwa Padre mwenyewe na kwa ajili ya familia ya Mungu inayomzunguka. Hapa kuna haja ya kuwa makini katika kuwachagua majandokasisi wanaoweza kuingia Seminarini tayari kuanza safari ya maisha na wito wa Kipadre, vijana hawa wanapaswa kuangaliwa kwa kina na mapana katika safari yao, ili waweze kusaidiwa kikamilifu bila ya kuwa na haraka wala kuchukua mambo kijuu juu tu!

Kardinali Stella anasema, hapa hakuna njia ya mkato, kila hatua inapaswa kushughuliwa kikamilifu pasi na haraka wala upendeleo, ili kuhakikisha ukomavu wa jandokasisi. Hapa lazima kuwepo na malezi endelevu yanayomsaidia Jandokasisi kupata mambo msingi katika maisha na utume wake wa Kipadre hapo baadaye. Kumbe, majiundo ya falsafa, taalimungu na shughuli za kichungaji yameboreshwa kwa kuongezewa tena majiundo ya kitume, utambulisho wa wito na utume wa Kipadre, ili kuweza kuwa na mwelekeo mkamilifu wa Yesu Kristo mchungaji mwema.

Padre mwema, mtakatifu na mchapakazi hapatikani kwa kufaulu vyema masomo na mitihani yake, bali anahitaji kuwa na ukomavu wa kiutu, maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji. Awe makini na lugha anayoitumia katika maisha na utume wake bila kusahau mbinu msingi za malezi na majiundo. Mambo makuu mawili yamepewa kipaumbele cha kwanza: Utu”, yaani, Majandokasisi wanapaswa kusindikizwa ili waweze kuwa na ukomavu katika utu wa binadamu, ili kweli waweze kupenda na kupendwa katika hali ya ukomavu; watu huru kutoka katika sakafu ya maisha yao; watu wanaoweza kujenga na kudumisha mahusiano ya kijamii; watu wenye amani na utulivu wa ndani; wanaoweza kutoa na kupokea na kumwilisha Mashauri ya Kiinjili katika maisha yao bila shuruti, unafiki wala kutafuta njia ya mkato.

Kardinali Stella anasema, “Tasaufi” ni neno la pili, lililopewa kipaumbele cha pekee katika malezi na majiundo ya kipadre kwa kufunda dhamiri nyofu mintarafu maisha na wito wa Kipadre. Ikumbukwe kwamba, Padre si mfanyakazi wa mshahara wala mfanyabiashara anayelitumia Kanisa kwa ajili ya mafao yake binafsi. Padre ni mfuasi wa Kristo Yesu anayejisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwa kujenga na kudumisha uhusiano wa pekee na Kristo kwa njia ya Neno, Sakramenti, Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na sadaka binafsi, kielelezo cha Kristo mchungaji mwema. Mapadre wanapaswa kuboresha maisha yao ya kiroho yanayofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili kwa kujisikia kuwa na Kanisa kwa ajili ya Kanisa kama alivyokuwa Kristo Yesu.

Mapadre wanapaswa kuwa ni watu wa “Huduma” yaani “Wasamaria wema”, watu wenye huruma, upendo na msamaha. Hawa ni watu wanaopaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kwani katika maisha na utume wao, watakutana na watu wenye kiu ya kusikilizwa; watu wanaweza kuanzisha na kudumisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi pasi ya kuwa na jazba au kutaka kulipiza kisasi. Ikumbukwe kwamba, ndani ya familia ya Mungu kuna watu ambao wamejeruhiwa vibaya wanapaswa kugangwa na kuponywa na huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, ushauri makini na ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Majandokasisi wanapaswa kuondokana na tabia ya kujifungia katika ubinafsi wao, tayari kujielekeza katika mwono mpana utakaowapatia mang’amuzi ya kina katika maisha na utume wao kwa siku za baadaye, kama Mapadre! Kardinali Stella anasema, dhamana kubwa iliyoko mbele yake kama Mweyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri ni kusali kwa ajili ya kuwaombea Wakleri, yaani: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu. Baadhi yao wanaishi na kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, kumbe wanahitaji kusindikizwa kwa njia ya sala na sadaka ili kamwe wasikate tamaa, hata pale wanapoteleza na kuanguka katika udhaifu wa kibinadamu wawe na ujasiri wa kusimama na kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Kanisa pia limebahatika kuwa na umati mkubwa wa Mapadre wema, watakatifu na wachapakazi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake bila hata ya kujibakiza, wote hawa wanapaswa kuungwa mkono ili waendelee kusonga mbele kwani mapambano baado kabisa yanaendelea hapa duniani, hadi kitakapoeleweka. Mapadre wajenge na kudumisha utamaduni wa maisha matakatifu katika utume wao wa Kipadre, kwa kuendelea kuboresha maisha yao ya kiroho kwa njia ya nyenzo ambazo zimewekwa na Mama Kanisa; waendelee kuwajibika barabara katika shughuli za kichungaji kwa kushirikiana na watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao.

Mapadre wawe makini na kuendelea kukesha daima katika sala, tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti na matendo ya huruma, na kamwe wasidhani kwamba wamekwisha kufika, bali wako safarini na bado kuna vishawishi na changamoto nyingi katika maisha na utume wa Kipadre! Siku ambapo Mapadre watabweteka, hapo watakiona cha mtema kuni! Upadre ni zawadi na wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu unapaswa kulindwa na kudumishwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.