2017-06-01 14:19:00

Watawa wanapaswa kuwa ni vyombo vya Injili ya upendo na furaha!


Shirika la Masista wa Bikira Maria Malkia wa Mitume, Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania limeadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth, kwa kuwashangilia watawa wake sita walioadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Maisha ya kitawa, kwa kutakiwa kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huduma na furaha kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria kwa binamu yake Elizabeth. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano katika maisha na utume wao kama watawa wanaohamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, tayari kushiriki katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Jubilei ni kipindi cha kushukuru kwa neema na baraka ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake, lakini ni muda pia wa kuomba toba na msamaha kutokana na mapungufu yaliyojiri katika maisha na utume wao kama watawa! Haya yamesemwa na Askofu Evarist Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya Watawa wa Shirika la Bikira Maria Malkia wa Mitume, Jimbo Katoliki Mbeya tarehe 31 Mei 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua. Amewataka watawa hawa kuiga mfano wa Bikira Maria aliyejitosa kuwa ni chombo cha huduma, upendo, furaha na faraja kwa binadamu yake Elizabeth.

Amewashauri watawa hawa kutumia muda wao kwa ajili ya kujitakatifuza, kwa kuambata neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Kristo na Kanisa lake. Jubilei ya miaka 25 iwe ni fursa ya kujifungamanisha zaidi na Mungu na kamwe wasiishi kwa mazoea! Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huduma, huruma na mapendo kwa jirani zao katika huduma ya elimu, afya, katekesi na huduma ya ustawi wa jamii, daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Watawa wasaidiane na kukamilishana kwa kurekebishana na kuonyana kwa upendo na udugu na kamwe wasikubali kumfungulia shetani malango ya maisha, wito na utume wao. Daima wajitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu kwa njia ya Katiba, Sheria, Kanuni na Miongozo ya Maisha ya Kitawa. Watawa wajenge na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati na kamwe wasiwe ni watu wa “kupika majungu” kwani majungu daima si mtaji, kama ungekuwa ni mtaji, bila shaka wangekuwa wametajirika wengi! Wajenge utamaduni wa kusema kweli, wazi na kwa heshima ya jirani zao.

Watawa wakati wa uchaguzi, wamwombe sana Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kuchagua kiongozi atakayewaongoza kadiri ya mapenzi ya Mungu, kwa kuonesha dira kwa mawazo, maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha! Watawa waendelee kujiimarisha katika uutakatifu wa maisha kwa njia ya sala, maisha ya kijumuiya, Sakramenti za Kanisa na tafakari makini ya Neno la Mungu. Changamoto za maisha wanaweza kuzikabili kwa kushikamana, kusaidiana na kukamilishana kama ndugu wamoja katika Kristo Yesu! Watawa walioadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Utawa ni Sr. Astrida Katimbuka, Sr. Asteria Nyamwela, Sr.Victoria Aswile, Sr. Yosepha Ayobangila, Sr. Adelphina Kipangula pamoja na Sr,Joyce Nchalla na Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Jimbo Katoliki la Mbeya.

Na Thompson Mpanji,

Mbeya, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.