2017-06-01 14:40:00

Siku kuu ya Pentekoste, Siku ya kuzaliwa kwa Kanisa!


Naam ndugu msikilizaji: “Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inaviungamanisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti, Aleluya!” Antifona ya wimbo wa mwanzo ndiyo inavyotufungulia sherehe ya Pentekoste, siku hamsini baada ya sherehe ya Pasaka. Pentekoste inahitimisha rasmi kiliturujia adhimisho la Pasaka. Ni sherehe ya kuzaliwa kwa Utume wa Kanisa. Mitume wanaanza rasmi utume wao ambao hadi leo umeenea ulimenguni kote na unaendelea kuimarishwa kila siku. Roho huyu ni ahadi ya Kristo kwa wafuasi wake kabla ya kupaa kwake kwamba watapokea Roho kutoka juu na hivyo kuwa mashahidi wa Kristo kwa ulimwengu wote (Mdo 1:8). Roho huyu ni msaada kwetu wanakanisa kwani kwa njia yake tunapokea nguvu na uwezo wa kimungu; huyu ni Roho ambaye “anaufanya upya uso wa dunia”.

Uwepo wa Roho Mtakatifu ni udhihirisho wa uwepo wa Mungu pamoja nasi. Uwepo huu wa Mungu unatufanya kuwa wamoja kulingana na hulka ya Mungu aliye mmoja. Historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu ilinuia kumrudisha mwanadamu katika umoja ambao uliharibiwa na dhambi. Dhambi ilimtukuza kiumbe na kumwondoa mwenyezi Mungu. Matunda yake ya mwanzo kabisa yalijidhihisha katika uhasama na kutoelewana kati ya wanadamu. Adamu alimlaumu mkewe Eva, Kaini akamuua ndugu yake Abeli na katika ujenzi wa mnara wa Babeli wanadamu wakaingia katika hali ya kutoelewana lugha kabisa. Hii yote inaonesha kwamba, bila uwepo wa Mungu uhalisia wa mwanadamu ambaye ameumbwa katika umoja kwa ajili ya kila mmoja kuwa msaidizi kwa mwenzake huaribiwa.

Somo la kwanza linatuonesha uhalisia wa jamii hii iliyogawanyika. Mgawanyiko kati ya wanadamu ni sababu ya kutoelewana na kila mmoja kujifanya mambo yake kama atakavyo yeye hata kama haeleweki kwa wengine. Lakini jamii tunayopewa mfano katika somo la kwanza inapokea jambo jipya. Upya huu unawashangaza sana; wanashindwa kuuelewa na kujiuliza inakuwaje mambo haya, hawa tunawafahamu ni kutoka mataifa mbalimbali lakini “tunawasikia wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu”. Roho Mtakatifu ambaye ni uwepo wa Mungu katikati ya wanadamu analeta uelewano. Wanadamu wanaungana tena. Pamoja na uwepo wa watu wa asili tofauti katika Yerusalemu, kushuka kwa Roho Mtakatifu kunawaunganisha na wanaelewana. Hii ni kwa sababu inabaki lugha moja, lugha ya kimungu, lugha ambayo inaeleweka katika kutenda yote katika muelekeo halisia uliokuwapo tangu uumbaji.

Tendo hili la kunena kwa lugha mbalimbali lakini katika hali ya kuelewana linaweza kutafsiriwa kama udhihirishwaji wa vipaji mbalimbali wanavyokirimiwa watu tofauti lakini wanapobaki katika kuvidhihirisha katika uwezo wa Roho Mtakatifu vinakuwa sababu ya kuunganisha watu wote. Jamii ya wanadamu katika nafasi mbalimbali iwe ni katika familia, katika jumuiya au katika taifa watatenda katika umoja na kujenga kitu kimoja kwa faida ya wote pale tu lugha yao hiyo inaposababishwa na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anatuletea lugha moja ya upendo na anatudhihirishia uwepo wa Mungu uliosheheni utajiri wa vipaji anuai vyenye lengo moja tu. Ni mwaliko wa kumkaribisha Roho Mtakatifu kusudi kutoa nafasi kwa kila mmoja kuchangia katika kujenga kitu kimoja, yaani ukombozi wa mwanadamu.

Jamii mamboleo ambayo inatawaliwa na ukanimungu inafanya bidii ya kumuondoa Mungu. Uwepo wa Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu unapokea mwitikio hasi. Hii ni sababu ya kuwa na jamii ya mwanadamu iliyogawanyika. Kila mmoja anaongea katika lugha yake ambayo hakuna anayeweza kuielewa. Hii inaleta athari kubwa sana katika mshikamano na umoja wa kibinadamu na matokeo yake ni mabaya katika juhudi za kuilinda au kuitetea hadhi ya mwanadamu. Maovu mengi dhidi ya binadamu mfano ajira za watoto, biashara za binadamu kwa ajili ya ukahaba, rushwa, utoaji wa mimba na mengineyo mengi ni matokeo ya muelekeo huu wa kisekulari. Kwa upande mwingine matukio ya vita ndani ya jamii moja au kati ya jamii moja na nyingine yanathibitisha kwamba wanadamu hawataki kuongea katika lugha moja inayoeleweka na wote.

Roho Mtakatifu analeta upatanisho kati ya Mungu na mwanadamu. Amani hii kati ya mwanadamu na Mungu inampatia fursa mwanadamu kupatana na mwanadamu mwenzake. Hii ni zawadi ya kwanza ya Kristo Mfufuka. Yeye aliwapatia amani: “Amani iwe kwenu”. Ni dokezo kwamba katika hali ya dhambi kunakosekana muunganiko kati ya Mungu na mwanadamu na kati ya mwanadamu na mwanadamu mwenzake. Upatanisho unaeletwa na Kristo unaleta amani na hivyo mwanadamu anaweza kuongea tena katika lugha itakayoeleweka na wenzake. Zawadi ya Roho Mtakatifu  ni ya faida kwa mwanadamu kwani chuki, uhasama, visasi na vinyongo vinaondoka kati yao. Wote wanatembea katika njia moja na hata ikitokea mmoja anakengeuka basi atarudishwa katika njia sahihi. Ujio wa Roho Mtakatifu ni jibu letu Wakristo kwa jamii ya mwanadamu ya kuimarisha umoja, upendo na mshikamano.

Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakorintho unatuasa kuuthibitisha umoja huo katika ushirikishanaji wa vipaji mbalimbali. Roho Mtakatifu ndiye mgawaji wa vipaji vyote. Tofauti zetu katika kutenda kazi zisitufanye kujiona kuwa bora kuliko wengine. Hakuna kazi au nafasi bora kwani kazi au nafasi haiongezi kitu katika ubinadamu wetu. Sote tunabaki kuwa sawa. Tunapoanza kujikweza kwa sababu ya kazi au nafasi yangu na dhahiri tunatenda si kwa kadiri ya karama tupewazo na Roho Mtakatifu bali kadiri ya ubinafsi wetu. Kiuhalisia mwanadamu ameumbwa kumtegemea mwingine. Daktari asijione kuwa ni bora zaidi ya mfuaji wa umeme ambaye anawezesha mitambo ya hospitali kutenda kazi sawasawa. Mwalimu hawezi kumdharau mtengeneza chaki au kalamu au daftari kwani bila zana hizo utekelezaji wa majukumu yake utakuwa mgumu. Roho Mtakatifu anatoa vipaji mbalimbali ili katika umoja na utofauti wake viweze kutegemezana na kukamilishana!

Ni wajibu wetu sisi Wakristo kutoa ushuhuda wa maisha yetu ya kikristo kwani “Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu, na Roho Mtakatifu tuliyepewa. Tuustawishe umoja wa kimungu ili uwe chachu kwa maisha ya kindugu kati yetu wanadamu. Tutoe ushuhuda wa kimaisha kwa kudhihirisha mshikamano kuanzia katika familia zetu hadi katika jamii yote kwa ujumla. Tutoe nafasi kwa kila mmoja kushiriki kulijenga Jiji la Mungu hapa ulimwenguni kwani Roho Mtakatifu anatenda kwa kila mmoja kwa namna mbalimbali kwa makusudi ya kutufikisha katika lengo moja.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.