2017-06-01 09:30:00

Roho Mtakatifu awatie nguvu na ujasiri wa kuwa mashuhuda amini!


Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kupata mapaji na karama mbali mbali zinazowafanya kuimarika katika ujasiri na matumaini na hatimaye, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Mfufuka katika maisha ya watu wanaowazunguka. Lakini, ili kweli waamini waweze kupokea Mapaji ya Roho Mtakatifu, hawana budi kuonesha juhudi kwa kumpenda Mungu kwa moyo na akili zao zote, kwani Mungu ni upendo na ni asili ya wema na utakatifu wote. Amri za Mungu ni dira, mwongozo na utambulisho wa familia ya Mungu katika hija ya maisha yake hapa duniani.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa hivi karibuni na Padre Alcuin Nyirenda, OSB katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwapongeza watanzania waliopata madaraja mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa; watawa walioweka nadhiri zao sanjari na kuwaaga watanzania waliohitimu masomo yao hapa Roma katika kipindi cha Mwaka 2016/2017 na sasa wanajiandaa kurejea nchini Tanzania kwa ajili ya kuwahudumia watanzania kwa unyofu, upole, ari na moyo mkuu kama kielelezo cha tumaini lililomo ndani mwao!

Padre Alcuin Nyirenda, anafafanua kwamba, Roho Mtakatifu ni “Msaidizi”, “jirani”, “wakili” “advocatus”, “ad - vocare” yaani “Mfariji” kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye Mfariji wa kwanza na Roho wa kweli na utukufu. Siku kuu ya Pentekoste ni siku ambayo Fumbo la Utatu Mtakatifu linafunuliwa kikamilifu; ufalme wa Mungu unakuwa wazi kwa watu wote wanaomsadiki Kristo Yesu katika hali ya unyenyekevu, imani na kushiriki katika maisha ya kiroho. Roho Mtakatifu anapowashukia Mitume, wanapata ujasiri wa kutangaza, kushuhudia na kutenda mambo makuu katika maisha ya watu.

Maajabu ya Mwenyezi Mungu yanatolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu. Roho Mtakatifu anawasaidia waamini katika udhaifu wao, lakini anasema Padre Alcuin sharti kuu ni kumpokea, kumkubali na kumpenda Kristo Yesu kwa moyo wote, tayari kushuhudia maisha na utume wake miongoni mwa familia ya Mungu. Watanzania waliopewa madaraja mbali mbali pamoja na kuhitimu masomo yao sasa wanayo hoja ya kusimulia kwa upoke na unyenyekevu matumaini yaliyomo ndani mwao. Kanisa linawatakia utume ufanisi mwema kadiri ya karama na mapaji ambayo wamekirimiwa na Roho Mtakatifu. Wajitahidi kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka kwa mfano bora wa maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.