2017-06-01 13:56:00

Kanisa linahitaji mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo!


Utume ni kiini cha imani ya Kikristo ndiyo kauli mbiu inayoongoza mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa uliofunguliwa tarehe 29 Mei na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 3 Juni 2017 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.  Akichangia mada katika mkutano huu, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anasema, Mwenyezi Mungu anapenda kuwashirikisha waamini katika maisha na utume wa Kristo Yesu, kwa njia ya imani inayowawezesha kutambua kwamba, wanaitwa na kutumwa na Mwenyezi Mungu ili kushiriki katika kutangaza na kushuhudia upendo wa huruma ya Mungu inayogeuza na kuokoa!

Kanisa linashiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia upendo wa huruma ya Mungu katika maisha na utume wake. Hakuna Jumuiya yoyote ya Kikristo inayoweza kujidai kwamba, imekamilika! Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa bado linasafiri kuelekea katika ukamilifu wake, kumbe, Injili itaendelea kutangazwa na kushuhudiwa; watu wataendelea kutubu na kuongoka, hadi kufikia utimilifu wake katika Fumbo la Ufufuko. Kumbe, utume, ni kiini cha imani ya Kikristo na kwamba, Kanisa daima linapaswa kupyaishwa kutoka katika undani wake; ndiyo maana, Kanisa bado linaendelea kukazia umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kuambata harufu ya utakatifu unaobubujika kutoka kwa watakatifu, wafiadini na waungama imani. 

Bila ushuhuda wenye mvuto na mashiko, Kanisa linaweza kuonekana kuwa kama NGO kwa kukusanya na kugawa rasilimali fedha na vitu kwa wahitaji. Kardinali Filoni anakazia kwa namna ya pekee, ushuhuda unaomwilishwa katika matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji. Ushuhuda huu ni ule unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, changamoto kwa Mama Kanisa kuendelea kuhamasisha ari na mwamko wa kimissionari.

Kardinali Filoni anasema, tarehe 30 Novemba 2019, Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume ujulikanao “Maximum Illud” unaopembua mchakato mzima wa shughuli za kimissionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Ni waraka unaokazia umuhimu wa maandalizi ya wamissionari na wakleri katika maisha na utume wa Kanisa; umuhimu wa mapadre, watawa na waamini walei kuchuchumilia utakatifu wa maisha pamoja na kuendelea kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei wanashirikishwa kwa namna ya pekee utume wa kimissionari kwa njia ya sala; kwa kusaidia kutegemeza miito mbali mbali ndani ya Kanisa sanjari na kuchangia kikamilifu katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa Mahalia.

Kardinali Filoni anakaza kusema, Mwezi Oktoba, 2019, utakuwa ni mwezi maalum kwa Mama Kanisa kujikita katika sala, matendo ya huruma, katekesi makini sanjari na tafakari ya kina kuhusu taalimungu na maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, wakristo wote wanahamasishwa kusaidia kuyategemeza Makanisa Mahalia, kiuchumi, ili kweli yaweze kusimama imara kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kumbe, hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kuchangia ukuaji wa Makanisa Mahalia, kwa kutambua kwamba, kila mwamini anaweza kuchangia kadiri ya uwezo na nafasi yake.

Katika mwelekeo huu, Baraza la Kipapa la uinjilishaji wa watu linaendelea kujipanga ili kuweza kuunganisha vyombo vyake vya habari kuwa ni chombo kimoja chenye nguvu zaidi, sanjari na kuendeleza mageuzi katika Sekretarieti kuu; kwa kukazia majiundo awali na endelevu ya wamissionari; umoja na mshikamano kwa Makanisa Mahalia kwa kuunganisha nguvu katika masuala ya: familia, uzazi na malezi bora; Injili ya uhai; elimu na shule; pamoja na kuendelea kujikita katika kuwalinda watoto wadogo, kwa kusaidia majiundo makini ya wazazi na walezi; mapadre, watawa na makatekista!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.