2017-05-31 15:28:00

Papa Francisko asikitishwa sana na shambulizi la kigaidi huko Kabul!


Watu 80 wamefariki dunia na wengine 350 kujeruhiwa vibaya kutokana na bomu la kujitoa mhanga kulipuka katika eneo la ofisi za mabalozi huko Kabul, nchini Afghanistan, Jumatano tarehe 31 Mei 2017. Wachunguzi wa mambo ya kijeshi wanasema, hili ni shambulio kubwa kuwahi kutokea nchini Afghanistan tangu mwaka 2014, hali inayotia shaka uwezo wa Serikali ya Afghanistan katika masuala ya ulinzi na usalama.

Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Balozi wa Afghanistan nchini Italia, anasema, anasikitishwa sana na taarifa za mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na wengine wengi waliojeruhiwa kutoka na vitendo vya kigaidi. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii kuungana na wote wanaoomboleza kwa kuondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zao, anawaombea marehemu wote pumziko na mwanga wa milele uweze kuwaangazia. Anawaombea majeruhi wote waweze kupona haraka na kurejea tena katika shughuli zao za kila siku! Anapenda kuwahakikishia wananchi wote wa Afghanistan sala zake kwa ajili ya amani na usalama nchini humo! Taarifa zinasema kwamba, balozi zilizoathirika na shambulizi hili la kigaidi ni: Ubalozi wa Ujerumani, Uingereza, Canada, China, Uturuki na Irani pamoja na ofisi mbali mbali za Serikali. Waathirika wakubwa kadiri ya taarifa ya serikali ni wanawake na watoto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.