2017-05-30 12:08:00

Jubilei ya Miaka 50 ya Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Duniani!


Kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Duniani kinafanyika mjini Roma kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 3 Juni 2017 kwa mkesha wa Siku kuu ya Pentekoste kwenye Uwanja wa Circo Massimo, Roma. Kilele cha maadhimisho haya ni Jumapili ya Pentekekoste kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican majira ya saa 4:30 kwa saa za Ulaya. Chama hiki nchini Italia kinaadhimisha pia kumbu kumbu ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwake. Kwa kutambua uzito wa tukio hili katika maisha na utume wa Kanisa, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu, hivi karibuni alimtumia ujumbe Dr. Salvatore Martinez, Rais wa  Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia, akiwatakia heri na baraka katika maadhimisho haya.

Maadhimisho ya Jubiliei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Uhamasho wa Kikatoliki Duniani ni fursa ya kumshukuru Roho Mtakatifu kwa mafuriko ya neema katika kipindi hiki chote ndani ya Kanisa, matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Tayari wajumbe kutoka ndani nan je ya Italia wameanza kuwasili tayari kushiriki katika semina, makongamano na sala katika makanisa mbali mbali hapa Roma. Ni wakati wa kusikiliza shuhuda za wanachama wa kwanza kwanza wa Uhamasho wa Roho Mtakatifu na changamoto walizobalina nazo kwa wakati huo.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, anawataka Wanachama wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia kubaki wakiwa wameshikamana kwa dhati katika upendo na kwamba, umoja huu unapaswa kuonekana. Kanisa linawataka kushuhudia mwanga wa ushuhuda huu unaopaswa kuwaangazia wote ili kamwe asiwepo mtu ambaye ananyimwa mwanga wa nguvu ya Injili. Baba Mtakatifu anawatakia mafanikio makubwa katika maadhimisho haya pamoja na kuendelea kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Anawaalika hata wao, kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.