2017-05-30 08:33:00

Askofu mkuu Protase Rugambwa: Utume ni kiini cha imani ya Kanisa!


Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” ni dira na mwongozo wa Mama Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kutambua kwamba, hii ni dhamana, kiini, maisha na utume wa Kanisa. Ili kufanikisha azma ya uinjilishaji mpya kuna haja ya kuwa na ujasiri wakufanya toba; mang’amuzi sanjari na mageuzi ya kweli kutoka miongoni mwa mihimili ya uijilishaji pamoja na taasisi wanazoziongoza na kuzisimamia kwa niaba ya Mama Kanisa! Haya ni ndiyo Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ambayo kuanzia tarehe 29 Mei hadi tarehe 3 Juni 2017 yanafanya mkutano wake wa mwaka mjini Roma kwa kuongozwa na kauli mbiu “Utume ni kiini cha imani ya Kikristo”. Mkutano huu umefungulizwa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ambaye pia ni Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu!

Katika hotuba yake elekezi, amewataka wajumbe kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro; waendelee kuhamasishana bila woga wala makunyanzi, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili. Ujumbe wa Kristo Mfufuka uliwezeshe Kanisa kuwa kweli ni Jumuiya ya watu wanaojipatanisha, wakarimu kwa jirani zao na wako tayari kutangaza na kushuhudia kazi ya wokovu miongoni mwa watu wa Mataifa! Katika mchakato wa uinjilishaji mpya anasema Askofu mkuu Rugambwa hakuna hata mmoja anayewekwa pembeni, bali wote ni sehemu ya kiini cha uinjilishaji, dhamana ambayo Kanisa limekabidhiwa na Kristo mwenyewe kwenda ulimwenguni ili kuwafanya wote kuwa ni wafuasi wake!

Askofu mkuu Rugambwa anasema, kuhusiana na bajeti na utekelezaji wa shughuli mbali mbali za Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa tayari muswada wa katiba utakao ratibu shughuli za  za ofisi pamoja na kuanzishwa kwa kamati ya fedha; kamati za majanga asilia na mkutano wa wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa katika ngazi ya Mabara, chombo muhimu sana katika kubadilishana, kutathmini, kujenga na kuimarisha huduma ya kitume pamoja na uhamasishaji wake tayari umekwisha andaliwa.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi ya kuadhimisha Mwezi Oktoba, 2019 kuwa ni mwezi maalum kwa ajili ya kumbuku mbu ya maadhimisho ya Miaka 100 tangu kuchapishwa kwa Waraka wa Kitume “Maximum illus" pamoja na kuendelea kujizatiti kwa Kanisa katika utume wake, mintarafu Waraka wa furaha ya Injili. Kwa sasa kuna kamati maalum inayoendelea kuboresha utambulisho wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa Kimataifa, kwa kuzingatia mahitaji ya Makanisa Mahalia.

Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa wanakumbushwa kwamba, wao ni wahudumu na wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu Mahalia katika huduma ya upendo kwa familia ya Mungu katika maeneo yao. Kumbe, wanapaswa kushiriki kikamilifu katika utume wa Mama Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa watu wa Mataifa kwa kushirikiana na Mashirika pamoja na vyama vya misaada kimataifa na kitaifa katika kupanga na kutekeleza mikakati ya huduma kwa familia ya Mungu.

Ili kufanikisha lengo hili, anasema Askofu mkuu Rugambwa kuna haja ya kuwa na mabadiliko ya dhati badala ya kuendelea na mtindo wa kurudia rudia yale yaliyotendwa kwa miaka iliyopita. Lazima, kipaji cha ubunifu, mang’amuzi, mwelekeo mpya, mitindo na mifumo mbali mbali iwasaidie kutambua kwamba, utume ni kiini cha imani ya Kikristo! Kumbe, shughuli nzina ya kuhamasisha shughuli za kimissionari, kukusanya na kugawanya rasilimali fedha kwa ajili ya mahitaji mbali mbali lazima; juhudi hizi zielekezwe katika wongofu wa kitume, tayari kujizatiti zaidi katika mchakato wa uinjilishaji mpya.

Askofu mkuu Rugambwa anakaza kusema, changamoto hizi zote hazina budi kufanyiwa tafakari ya kina, kupembuliwa kwa dhati na kumwomba Roho Mtakatifu, ili aweze kuwasaidia kuwa na mwelekeo mpya, ari na nguvu mpya katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Mwelekeo wa mawazo na fikra ni muhimu sana katika utekelezaji wa dhamana na majukumu ya Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa. Kipaumbele kiwe ni kwa ajili ya mambo msingi kwa ajili ya utume wa Kanisa na wala si vinginevyo! Wongofu wa kitume, utawawezesha kujenga Jumuiya za Kikanisa, umoja na udugu vinavyomwilishwa katika huduma ya uinjilishaji unaookoa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.