2017-05-28 15:02:00

Wakleri na watawa wanataka kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili!


Kardinali Angelo Bagnasco, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Genova, Jumamosi, tarehe 27 Mei 2017 alipata nafasi ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko ili kuzungumza na wakleri, watawa; viongozi wa dini na madhehebu ya Kikristo pamoja na wafanyakazi kutoka katika ofisi za majimbo ya Liguria, ili aweze kuwapatia neno litakalowasaidia kusonga mbele katika maisha na utume wao, daima wakijitahidi kujenga umoja, udugu na urafiki unaowawezesha kutembea pamoja bila woga wala wasi wasi. Lakini mkazo zaidi ni toba na wongofu wa ndani unaofumbatwa katika maisha ya mtu binafsi na wongofu wa shughuli za kichungaji kama njia muafaka ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha.

Kardinali Angelo Bagnasco anapenda kumhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wamepokea changamoto inayowataka kutoka kifua mbele ili kutangaza na kumshuhidia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na mshikamano na maskini, wakimbizi na wahamiaji. Liguria inakadiriwa kuwa na Mapadre 600 wa Majimbo na 600 wa Mashirika na kwamba, kuna zaidi ya watawa 2, 000 wanaojisadaka usiku na mchana kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa kwa kuzingatia mambo msingi pamoja na kushirikiana katika huduma za kichungaji. Wanapenda kumhakikishia sala, upendo na uaminifu kwake yeye kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.