2017-05-28 13:24:00

Papa Francisko: majibu ya mateso ya binadamu yametundikwa Msalabani


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 27 Mei 2017 ametembelea Hospitali ya Watoto ya “Giannina Gaslini” iliyoko mjini Genova na kuandika maneno ya shukrani katika kitabu cha wageni mashuhuri. Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wagonjwa wanaoonjeshwa: huruma, upendo na tiba. Anawashukuru kwa kazi hii kubwa, utu na ubinadamu wao pamoja na faraja wanayoitoa kwa ajili ya watoto wagonjwa. Amewaomba kumkumbuka na kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa watoto wagonjwa, wazazi na walezi wao pamoja na wafanyakazi wote wa hospitali hii, amewashukuru wote kwa kusema, amependa kuwatembelea, ili kuwafariji katika mateso na mahangaiko yao, kwani magonjwa ni changamoto pevu ambayo hata wakati mwingine si rahisi sana kuweza kuipokea na kuikubali. Kuna swali ambalo halina majibu ya haraka haraka katika maisha, eti kwa nini watoto wanateseka na kusumbuliwa na magonjwa? Majibu ya swali hili tete anasema Baba Mtakatifu yametundikwa juu ya Msalaba, kwa kumwangalia Yesu Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa wafu!

Hospitali ya Watoto ya “Giannina Gaslini” iliyoko mjini Genova inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 80 ya huduma kwa watoto wadogo; kwa kujikita katika tiba na tafiti makini za magonjwa ya watoto. Baba Mtakatifu amewapongeza na kuwashukuru wote wanaoendelea kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Anawapongeza kwa urafiki, uelewa, sadaka na majitoleo yao kama baba na mama wa watoto hawa wagonjwa.

Hiki ni kielelezo cha upendo aliokuwa nao Senate Gerolamo Gaslini, muasisi wa Hospitali hii, aliyeamua kujisadaka kwa ajili ya kumbu kumbu endelevu ya mtoto wake aliyefariki dunia akiwa na umri mdogo sana! Ni hospitali ambayo imejijengea heshima na jina kubwa ndani na nje ya Italia, kama chemchemi ya ukarimu na mshikamano. Ni hospitali inayosimikwa katika imani ya Kanisa Katoliki kama faraja kwa wale wote wanaoteseka. Ni Injili ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Huu ni ushuhuda wa mtu aliyesukumwa na cheche za Injili kiasi kwamba, amegeuka kuwa ni Msamaria mwema na kwamba, wale wanaowahudumia wagonjwa kwa huruma na upole wanamhudumia Kristo Yesu anayewafungulia Ufalme wa Mbinguni. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Hospitali hii itaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake katika huduma ya tiba na tafiti za magonjwa, kwa msaada wa wale wote wanaoguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watoto wadogo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.