2017-05-28 13:08:00

Hija ya Papa Francisko Jimboni Genova ni tukio la kiimani!


Kardinali Angelo Bagnasaco, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Genova, Jumamosi, tarehe 27 Mei 2017 amempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea, kuwasikiliza na kuadhimisha pamoja na familia ya Mungu mjini Genova Mafumbo ya Kanisa. Uwepo wake kati yao unaendelea kuimarisha mshikamano, umoja na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa kutambua kwamba, Papa Benedikto XV alikuwa ni mwenyeji na mzaliwa wa maeneo haya. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Genova imejiandaa kikamilifu kwa tukio hili la kiimani ili liweze kuacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu.

Kardinali Bagnasco anawashukuru wadau wote waliofanikisha maandalizi na hatimaye maadhimisho haya kutoka Vatican na Genova, iliyosaidia kukuza na kudumisha moyo ari ya kushirikiana katika umoja. Waamini wamejiandaa kwa sala, katekesi na matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na athari za mkikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa; huduma ambayo imefanyika katika hali ya ukimya mkuu na sala ili kufikiri, kuamua na kutenda kwa pamoja.

Licha ya ukanimungu na kutopea kwa imani, lakini imani inaendelea kushamiri kwa kujikita katika Neno, Mafundisho ya Mababa wa Kanisa na maisha ya Kisakramenti kama chachu ya kukoleza mchakato wa uinjilishaji mpya. Ushiriki wa waamini walei umekuwa ni kivutio kikuu. Familia ya Mungu Jimboni humo inaendelea kujielekeza zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji. Vijana wanaendelea kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa, ili kukua na kukomaa katika imani, tayari kuzima kiu ya watu wa familia ya Mungu Jimbo ni Genova. Kardinali Bagnasco anamshukuru baba Mtakatifu Francisko kwa kusaidia kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo kwa wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.