2017-05-27 08:00:00

Usipokuwa na hoja ya kujibu kile unachoamini huo ni ushirikina!


Jumuiya ya watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma, hivi karibuni iliadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa baadhi ya watanzania kupata madaraka mbali mbali yaani Daraja ya Ushemasi wa mpito pamoja na Daraja ya Upadre bila kuwasahau baadhi ya watawa walioweka nadhiri zao za muda na za daima katika mashirika mbali mbali nchini Italia. Ibada ya Misa iliongozwa na Padre Alcuin Nyirenda, OSB aliyekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwani maisha ya wakfu yanayoendelea kustawi na kushamiri ndani ya Kanisa ni matunda ya Roho Mtakatifu, Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Amewashukuru na kuwapongeza Mashemasi wapya Charles Kato Rubaza kutoka Jimbo Katoliki la Geita, Shemasi Jonathan Wilfred Mkwizu kutoka Jimbo Katoliki la Same pamoja Padre Danstan Mushobolozi aliyepewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 13 Mei 2017 katika Parokia ya Kristo Mfufuka, Ishozi, Jimbo Katoliki Bukoba na Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo hilo. Mashemasi wamekumbushwa kwamba, wao wanapaswa kuendeleza Injili ya huduma kwa familia ya Mungu, lakini kwa kutambua kile wanachokifanya, wakiwa tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililoko ndani yao, lakini kwa upole na hofu kuu! Kushindwa kufanya hivi ni ushirikina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.