2017-05-27 15:10:00

Papa: Shambulizi la kigaidi huko Misri ni kitendo cha kinyama sana!


Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambi rambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa vatican, kwenda kwa Rais Abdel Fattah Al Sisi wa Misri, anasema, amesikitishwa sana na mauaji ya kinyama ya waamini 29 wa Kanisa Kikoptik nchini Misri, ambao wengi wao walikuwa ni watoto wadogo yaliyotokea Ijumaa, tarehe 26 Mei 2017. Haya ni mauaji ambayo yamefanyika kutokana na chuki za kidini zisizokuwa na mashiko hata kidogo. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wale wote walioguswa na msiba huu mzito! Anapenda kuwaombea marehemu ili waweze kupata pumziko la milele na kuonja huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito sala na sadaka yake. Anawaombea majeruhi ili waweze kupona haraka na kurejea tena katika maisha yao ya kila siku. Anaendelea kuombea mchakato wa amani, upatanisho na maridhiano kati ya wananchi wa Misri.

Baba Mtakatifu pia anapenda kuhamikishia Papa Tawadros II uwepo wake wa karibu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Salam za rambi rambi zimetolewa pia na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Anasema, inasikitisha kuona damu ya mahujaji wa amani inamwagika na wayu wasiokuwa na hatia wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na chuki za kidini. Familia ya Mungu nchini Misri inapaswa kuungana na kusimama imara dhidi ya misimamo mikali ya kidini; kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Wanaiomba Serikali ya Misri kuwashughulikia kisheria watu wote wanaosababisha mauaji ya kinyama kwa watu wasiokuwa na hatia

Askofu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani anasema, anapenda kuungana kwa njia ya sala na wale wote wanaoomboleza msiba mkubwa wa mauaji ya kinyama yaliyotokea huko Misri. Wote walioguswa na msiba huu waonje uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati ili kusitisha mauaji ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Kwa upande wake Patriaki Kirill wa I wa Moscow na Russia nzima anapenda kutuma salam zake za rambi rambi kwa Papa Tawadros II kufuatia msiba huu mzito wa mauaji ya watoto wasiokuwa na hatia. Mashambulizi haya ya kigaidi yasiwe ni kikwazo katika mchakato wa kutafuta haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Misri.

Kardinali Daniel N. DiNardo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani anaungana na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya kusali ili kuwaombea watu waliouwawa kikatili, Ijumaa tarehe 26 Mei 2017. Damu ya watoto hawa iwe ni ushuhuda wa imani ya Kikristo na jitihada za kutaka kujenga jamii inayosimikwa katika majadiliano ya kidini, ili kulinda, kujenga na kudumisha haki msingi za binadamu sanjari na uhuru wa kuabudu. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao yake makuu mjini Roma, inawaalika waamini wa Makanisa yote pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana nao ili kuomboleza msiba huu mzito uliowapata waamini wa Kanisa ka Kikoptik. Kuna haja ya kuongeza nguvu katika mchakato wa mapambano dhidi vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.