2017-05-27 14:58:00

Papa Francisko: Ninakuja kwenu Genova kama mtoto wa wahamiaji!


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, asubuhi, 27 Mei 2017 ameanza hija yake ya kichungaji Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia kwa kuwakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, anakwenda kati yao kama mtoto wa wahamiaji waliopata bahari kutumia bandari ya Genova kujipatia maisha bora zaidi huko Argentina. Anasema, anakwenda Jimboni mwao kama hujaji wa amani na matumaini. Anatambua fika kwamba,  Genova ni mji wa watu wakarimu, usiowafungia watu malango ya matumaini; ni mji unaojizatiti katika kuwakirimia watu mbali mbali wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kichungaji Jimboni humo, amebahatika kukutana na kuzungumza na ulimwengu wa wafanyakazi, akasikiliza kwa makini kilio cha ona kuwapatia neno la faraja. Amekutana na kuzungumza na wakleri, watawa na viongozi wa madhehebu na dini mbali mbali. Amezungumza na vijana waliokuwa wamefurika kwa wingi ndani na nje ya Madhabahu ya Bikira Maria Mlinzi, akapata chakula cha mchana na maskini, wakimbizi, wahamiaji na wafungwa. Baadaye amekwenda kuwatembelea na kuwafariji watoto wagonjwa kwenye Hospitali ya Gaslini na hatimaye, kiini cha hija hii kimekuwa ni Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa “Fiera del Mare”.

Baba Mtakatifu katika ujumbe uliochapishwa kwenye Jarida la Secolo XIX anasema, anakumbuka kwa namna ya pekee, ukarimu wa wananchi wa Genova kwa ndugu zake, ambao kunako tarehe 1 Februari 1929 walipanda Meli ya “Giulio Cesare: Mzee Giovanni na Rosa; Babu na Bibi yake pamoja na Mzee Mario ambaye wakati ule alikuwa na umri wa miaka 21. Anakwenda Genova kama mtoto wa wahamiaji na kwamba, anapenda kuchuku fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa moyo wao wa ukarimu na upendo. Baba Mtakatifu Francisko anatambua kwamba, wanayo matatizo, changamoto na fursa makini: Anafahamu kwamba, kuna idadi kubwa ya vijana wa kizazi kipya haina fursa ya ajira; kuna familia zinazoishi katika shida na mahangaiko makubwa. Familia ya Mungu mjini Genova inajishughulisha pia katika uvuvi, changamoto mbele yao ni kutweka hadi kilindini ili kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.